Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 27 Januari, 2021 amezindua Shamba la Miti lililopo katika Wilaya ya Chato Mkoani Geita na kuagiza shamba hilo liitwe Shamba na Miti Silayo ikiwa ni kutambua jitihada za Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) Prof. Dosantos Silayo katika uanzishaji wa shamba.
Shamba hilo lenye ukubwa wa Hekta 69,000 limeanzishwa mwaka 2017 ikiwa ni jitahada za TFS kuitikia wito uliotolewa na Mhe. Rais Magufuli wa kuitaka wakala hiyo kuongeza malighafi zitokanazo na misitu ambapo iliamua kubadili lililokuwa pori la Biharamulo/Kahama kuwa shamba la miti baada ya pori hilo kuharibiwa vibaya kutokana na kuvamiwa na wananchi waliokuwa wakiendesha shughuli mbalimbali zisizo za uhifadhi.
Shamba la Miti Silayo linakuwa shamba la pili kwa ukubwa hapa nchini likitanguliwa na Shamba la Miti la Sao Hill lililopo Mkoani Iringa lenye ukubwa wa zaidi ya Hekta 135,903, na linafanya jumla ya idadi ya mashamba ya miti ya Serikali hapa nchini kufikia 23 yenye ukubwa wa hekta 500,000.
Kamishna wa Uhifadhi Prof. Dosantos Silayo amesema miti takribani 29,000 imeshapandwa katika Shamba la Miti Silayo tangu miaka 4 iliyopita na kwamba shamba hilo limetoa ajira 800 kwa wananchi.
Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Damas Ndumbaro amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuandika historia ya kuwa Rais wa Kwanza kuzindua shamba la miti, na ameeleza kuwa sekta ya misitu ambayo katika mwaka uliopita ilichangia shilingi Bilioni 130 katika pato la Taifa na shilingi Bilioni 373 katika miaka 3 iliyopita imekuwa na mchango mkubwa katika kuinua kipato cha wananchi akitolea mfano wa halmashauri ya Wilaya ya Mafinga ambayo mwaka jana ilijipatia shilingi Bilioni 1.3 kutokana na misitu.
Kwa upande wake, Mhe. Rais Magufuli ameipongeza TFS kwa jitihada kubwa za upandaji miti katika misitu na mashamba mbalimbali hapa nchini na amesema ameamua lililokuwa Shamba la Miti Chato liitwe Shamba la Miti Silayo kwa sababu amejionea jitihada kubwa zilizofanywa na Prof. Silayo katika kulinusuru lililokuwa pori la Biharamuro/Kahama kwa kulifanya shamba la miti ambalo licha ya kuhifadhi mazingira, kuondoa hewa ukaa, kuzalisha malighafi za misitu na kuhifadhi maji litasaidia kuinua maisha ya wananchi bila kuwabagua kwa elimu zao.
Mhe. Rais Magufuli ameitaka TFS kuongeza kasi ya upandaji wa miti ili hekta zote 69,000 za shamba hilo zipandwe, kuweka mikakati mizuri ya uhifadhi wa shamba hilo na kusimamia vizuri rasilimali ya misitu katika maeneo mbalimbali nchini kwa kuhakikisha misitu inainufaisha nchi badala ya kuwanufaisha watu wachache ambao wanasafirisha magogo kwenda nje ya nchi badala ya kusafirisha mazao ya misitu yaliyoongezwa thamani zikiwemo samani.
Ameiagiza TFS na wadau wengine zikiwemo wizara na taasisi za Serikali kuweka mikakati ya kuwawezesha vijana wa Tanzania kunufaika na mazao ya misitu wakiwemo mafundi seremala pamoja na kuandaa miundombinu ya uchakataji wa mazao ya misitu vikiwemo viwanda vya mbao badala ya kusubiri mpaka uvunaji uanze.
Mhe. Rais Magufuli amewashukuru wananchi kwa kuridhia eneo hilo kuanzishwa shamba la miti na ameziagiza halmashauri na taasisi mbalimbali nchini kuhimiza upandaji wa miti katika maeneo yao.
Amewathibitishia wananchi wa Buseresere na Katoro kuwa ahadi yake ya kuanzisha Wilaya mpya ipo palepale kwa kuwa eneo hilo lina kila sababu ya kuwa na Wilaya yake na ameziagiza mamlaka zinazohusika kuanzisha mchakato huo.
Akiwa njiani kutoka Geita kwenda Kahama Mkoani Shinyanga, Mhe. Rais Magufuli amewasalimu wananchi wa Nampalahala, Runzewe na Ushirombo ambapo amemuagiza Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso kushughulikia haraka changamoto za maji zinazoyakabili maeneo hayo na amewahakikishia wananchi hao kuwa vijiji ambavyo havijapata umeme vitapatiwa umeme ndani ya miaka miwili kuanzia sasa.
Mhe. Rais Magufuli amefungua majengo ya Kituo cha Afya cha Masumbwe kilichopo katika Wilaya ya Mbogwe ambayo yamegharimu shilingi Milioni 400 na ameahidi kuwa baada ya kupeleka shilingi Milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya, Serikali itaongeza fedha nyingine shilingi Milioni 500 kwa ajili ya ujenzi huo na ametoa wiki 1 kwa TAMISEMI kutangaza zabuni ya ujenzi wa barabara ya lami ya kilometa 1.2 inayounganisha kituo cha Afya cha Masumbwe na barabara kuu.
Ameiagiza Wizara ya Afya kuangalia uwiano wa mgawanyo wa dawa hapa nchini kutokana na kutoridhishwa na ongezeko dogo la fedha za dawa zilizopelekwa Mkoani Geita ambapo zimeongezeka kutoka shilingi Bilioni 2.35 hadi shilingi Bilioni 2.75 kwa mwaka ilihali kuna ongezeko kubwa la bajeti ya dawa nchini nzima la kutoka shilingi Bilioni 31 hadi kufikia shilingi Bilioni 270 kwa mwaka.
Kuhusu malalamiko ya wananchi kuporwa ardhi baada ya maeneo yao kupatiwa wawekezaji wa kuchimba madini, Mhe. Rais Magufuli ameagiza viongozi wote kusimamia vizuri sheria zinazotoa haki ya ardhi kwa wananchi, badala ya kuwaacha wawekezaji wakichukua maeneo ya wananchi kwa kutumia sheria za madini pekee.
Mhe. Rais Magufuli ambaye ameongozana na Waziri wa TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo, Waziri wa Madini Mhe. Doto Biteko, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhandisi Elias Kwandikwa, Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso na Waziri wa Afya Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima kesho ataendelea na ziara yake hapa Kahama Mkoani Shinyanga ambapo ataweka jiwe la msingi la Ofisi ya Halmashauri ya Mji wa Kahama, ataweka jiwe la msingi la jengo la matibabu ya nje (OPD) la Hospitali ya Wilaya ya Kahama na ataweka jiwe la msingi la viwanda vya vinywaji, nafaka na maziwa, na atazungumza na wananchi wa Kahama katika uwanja wa Taifa wa Halmashauri ya Wilaya ya Kahama.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Kahama
27 Januari, 2021.