Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Rais Magufuli Apiga Kura kwa Kufuata Utaratibu
Oct 28, 2020
Na Msemaji Mkuu

Na. Immaculate Makilika - MAELEZO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. John Pombe Magufuli amepiga kura katika kituo cha Ofisi ya Idara ya Maji kijiji cha Chamwino Ikulu kata ya Chamwino, Dodoma ambapo alipanga foleni kwa takriban dakika kumi kabla ya kupiga kura.

Rais Magufuli aliwataka watanzania kujitokeza kwa wingi kupiga kura ili kutimiza haki yao ya kuchagua viongozi wanaoona wanafaa.

“Leo ni siku muhimu sana katika kukuza demokrasia katika taifa letu, wito wangu kwa watanzania tujitokeze kwa wingi kwenda kupiga kura kwa ajili ya kufanya maamuzi ambayo kila mmoja atakuwa nayo katika moyo wake”, alisema Rais Magufuli.

Aidha, aliwataka watanzania kutekeleza jukumu hilo kwa utulivu na amani kwani yapo maisha baada ya uchaguzi.

Katika hatua nyingine, Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Hussein Mwinyi naye ameonekana kufuata utaratibu wa kupanga foleni na baadae kupiga kura ambapo amewahimiza Wazanzibar kuendelea kujitokeza kupiga kura na kutimiza haki yao hiyo ya kikatiba.

Naye, Mgombea Urais kupitia Chama cha ADC, Queen Sendiga, ambaye amepiga kura eneo la Ununio, jijini Dar es Salaam, alisema kuwa amefurahishwa na utaratibu ulioandaliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na hivyo kuwataka watanzania kuendelea kupiga kura kwa amani.

Aidha. Sendiga aliongeza kuwa atafurahi endapo watanzania watamchagua katika nafasi hiyo ya urais kwani amaejipanga kuwaletea maendeleo kwa kutatua changamoto zilipo.

“Endapo watanzania hawatanichangua kwa nafasi hiyo ya urais bado nitaendelea kuwatumikia kwa nafasi niliyonayo  ya Naibu Katibu Mkuu wa ADC”, alisema Sendiga.

Hali ya amani na utulivu imeendelea kutawala katika maeneo mbalimbali ambapo watanzania wameendelea kuchagua viongozi wao.

Mwisho

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi