Ndege ya tatu ya Bombadier 8 Dash Q-400 ikipigiwa saluti ya maji baada ya kutua katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere ikitokea Montreal, Canada, na kupokelewa na umati mkubwa wa wananchi wakiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli leo Aprili 2, 2018
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 02 Aprili, 2018 ameongoza mapokezi ya ndege mpya aina ya Bombardier Dash-8 Q400 iliyonunuliwa na Serikali ya Tanzania kwa ajili ya Shirika la Ndege la Taifa (ATCL) ambayo imewasili hapa nchini ikitokea nchini Canada ilikotengenezwa.
Mapokezi ya ndege hiyo yenye uwezo wa kubeba abiria 76 yamefanyika katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Mawaziri, Wabunge, viongozi wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, viongozi wa dini, wakuu wa mikoa ya Dar es Salaam, Kilimanjaro na Mwanza na wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Akiwa uwanjani hapo Mhe. Rais Magufuli pamoja na viongozi na wananchi waliohudhuria mapokezi hayo wameshuhudia ndege hiyo ikipokea heshima ya kumwagiwa maji (Water Salute) na baadaye kuikagua.
Rais Dkt. John Pombe Magufuli akiwaongoza Viongozi wengine wa Serikali kukata utepe kuashiria uzinduzi wa ndege mpya ya Serikali aina ya Bombadier Dash-8 Q400 iliyowasili leo Jumatatu April 2, 2018 Jijini Dar es Salaam.
Katika hotuba yake Mhe. Rais Magufuli amewapongeza Watanzania kwa mafanikio haya makubwa ya kununua ndege kwa ajili ya kuliimarisha Shirika la Ndege la Taifa na kukuza utalii, na amewataka kuendelea kushikamana na kushirikiana na Serikali katika juhudi za mbalimbali za maendeleo.
Kabla ya hotuba hiyo viongozi wa dini wameiombea dua Tanzania na viongozi wake, na wamemtaka Mhe. Rais Magufuli kuendelea kufanya kazi zenye manufaa kwa Watanzania bila kujali wanaobeza juhudi hizo.
Hii ni ndege ya 3 kuwasili nchini kati ya ndege 6 zilizonunuliwa na Serikali, ndege nyingine kubwa 2 aina ya Bombardier CS300 yenye uwezo wa kubeba abiria 132 kila moja, na 1 aina ya Boeing 787-8 Dreamliner yenye uwezo wa kubeba abiria 264 zitawasili baadaye mwaka huu.
Mapema kabla ya mapokezi ya ndege hiyo Mhe. Rais Magufuli amezindua mradi wa kusimika mfumo wa rada 4 za kuongozea ndege za kiraia kwenye viwanja vya ndege vya Julius Nyerere, Kilimanjaro, Mwanza na Songwe, sherehe ambazo zimefanyika katika uwanja wa ndege kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Akitoa maelezo ya mradi huo Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga (TCAA) Bw. Hamza Johari amesema mradi huo ambao umeanza kutekelezwa tarehe 22 Agosti, 2017 utakamilika mwezi Mei 2019 kwa gharama Shilingi Bilioni 67.3 fedha zote zikiwa zimetolewa na Serikali ya Tanzania, na kwamba tayari utengenezaji wa rada ya kwanza ya uwanja wa Julius Nyerere umekamilika.
Amebainisha baadhi ya faida za mradi huo kuwa ni kuwezesha anga la Tanzania kuonekana kwa asilimia 100, utaiwezesha TCAA kutoa huduma kwa haraka na kuongeza mapato yatokanayo na tozo kwa ndege zinazopita katika anga la Tanzania, kuimarisha usalama na kuongeza uwezo wa TCAA kuongoza ndege nyingi na kwa haraka.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa Mnyaa amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa dhamira yake ya kuimarisha usafiri wa anga ikiwemo kutoa fedha kwa ajili ya kutekeleza mradi wa usimikaji wa rada 4, kujenga na kuboresha viwanja vya ndege nchini na kununua ndege mpya 6 kwa ajili ya kuimarisha usafiri wa anga.
Akizungumza kabla ya kuzindua mradi huo Mhe. Rais Magufuli ameipongeza TCAA kwa kuchangia asilimia 45 ya gharama za mradi huo kutokana na mapato yake na amemtaka mkandarasi anayejenga mradi huo kuukamilisha haraka ili kuondokana na hali ya sasa ambapo rada iliyopo ina uwezo wa kufanya kazi kwa asilimia 25 tu ya nchi nzima.
Mhe. Rais Magufuli amesema Watanzania wana kila sababu ya kutembea kifua mbele kwa kuwa nchi inakwenda vizuri na amewataka kuendelea kulipa kodi.
“Napenda kuwahakikishia kuwa tunakwenda vizuri, hivi sasa nchi yetu ni kati ya nchi 5 zenye uchumi unaokua kwa kasi Barani Afrika, tumechukua hatua katika sekta ya madini na sasa inachangia asilimia 17 ya pato la Taifa ikilinganishwa na asilimia 11 za huko nyuma.
“Nataka kuwahakikishia kuwa Serikali ipo, haijalala na haitalala” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
02 Aprili, 2018