Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

JPM Afuta Umiliki wa Mashamba Tanga
Aug 03, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na: Jacquiline Mrisho

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amefuta umiliki wa mashamba matano yenye jumla ya hekari 14,000 yaliyoshindwa kuendelezwa na wamiliki wake katika Wilaya ya Muheza mkoani Tanga.

Hatua hiyo imechukuliwa leo na Rais Magufuli wakati akiwahutubia wananchi wa Wilaya hiyo alipokuwa anapita kuelekea Tanga kwa ajili ya shughuli ya uwekaji wa jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa bomba la kusafirishia mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga,Tanzania.

Rais amefuta umiliki huo baada ya baadhi ya wananchi wa wilaya hiyo waliopewa mashamba hayo kwa ajili ya kuwekeza katika miradi mbalimbali ya kilimo ambacho kingeiingizia Serikali mapato, kuyaacha maeneo hayo bila kufanya uwekezaji tarajiwa.

“Tayari nimeshafuta umiliki wa mashamba matano yaliyokuwa yamechukuliwa bila kuendelezwa, nimeyarudisha kwa uongozi wa Mkoa ili wayapange maeneo hayo kwa ajili ya shughuli za Serikali pamoja na kuyagawa kwa wananchi. Nasisitiza wananchi wagaiwe mashamba hayo bure,” alisema Rais Magufuli.

Rais Magufuli ameongeza kuwa ardhi ya mkoa wa Tanga haikupangwa kwa ajili ya wawekezaji bali ni ardhi kwa ajili ya wananchi wote hivyo wana haki ya kupewa bure ardhi hiyo iliyoshindwa kuendelezwa.

Katika safari hiyo ya kuelekea Tanga mabapo alisimama maeneo mbalimbali kuwahutubia wananchi, Rais Magufuli alimpongeza Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Mhandisi Robert Gabriel kwa kutumia vizuri fedha za Serikali kuhamasisha vikundi vya wananchi kujenga madarasa kwa gharama ndogo na kuwataka viongozi wengine kuiga mfano wake.

Alipopewa nafasi ya kuwasalimia wananchi, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema kuwa utekelezaji wa maagizo mbalimbali ya Rais Magufuli unaonesha wazi dhamira yake ya kutaka kuifanya Tanzania kuwa mpya hivyo ni jukumu la kila Mtanzania kuhakikisha hamkatishi tamaa Rais Magufuli kwa kufanya kazi kwa bidii.

“Tunampongeza Rais Magufuli kwa juhudi zake za kuibadilisha Tanzania, katika bajeti ya sekta ya afya ya mwaka huu, tumepewa shilingi milioni 650 kwa ajili ya kuimarisha kituo cha afya cha Mkuzi, kikubwa ninaomba mtusaidie kuwaibua wanaouza dawa za Serikali ili tukomeshe tabia hii,” alisisitiza Waziri Ummy.

Baadhi ya maeneo ambayo Rais alisimama kuongea na wananchi wakati akielekea Tanga ni pamoja na Mkata, Michungwani, Hale, Muheza na Mkanyageni.

Rais Magufuli pamoja na Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda wanatarajiwa kuweka Jiwe la Msingi katika mradi mkubwa wa ujenzi wa bomba la mafuta la kutoka Hoima nchini Uganda mpaka Tanga, Tanzania. Jiwe hilo la msingi litawekwa eneo la Chongoleani lililopo Barabara ya Horohoro kuelekea Mombasa nje kidogo ya jiji la Tanga.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi