Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Rais Magufuli Afanya Mabadiliko Madogo ya Baraza la Mawaziri, Afanya Uteuzi wa Viongozi Mbalimbali
Jan 08, 2019
Na Msemaji Mkuu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 08 Januari, 2019 amefanya mabadiliko madogo katika Baraza la Mawaziri na kufanya uteuzi wa viongozi mbalimbali wa wizara na taasisi za Serikali.

Uteuzi wa viongozi hao uliotangazwa na Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi John Kijazi, Ikulu Jijini Dar es Salaam ni kama ifuatavyo;

  1. Rais Magufuli amemteua Mhe. Anjellah Kairuki kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji.

Mhe. Rais Magufuli amefanya uteuzi wa Waziri anayeshughulikia masuala ya uwekezaji kwa lengo la kuongeza msukumo na kuimarisha usimamizi wa masuala ya uwekezaji hasa baada ya kuamua Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kihamishiwe Ofisi ya Waziri Mkuu.

Kabla ya uteuzi huo Mhe. Kairuki alikuwa Waziri wa Madini.

  1. Rais Magufuli amemteua Mhe. Doto Biteko kuwa Waziri wa Madini. Kabla ya uteuzi huo Mhe. Biteko alikuwa Naibu Waziri wa Madini.

Kufuatia uteuzi huo Wizara ya Madini sasa itakuwa na Naibu Waziri mmoja ambapo Mhe. Stanslaus Nyongo anaendelea na wadhifa wake.

  1. Rais Magufuli amemteua Mhandisi Joseph Nyamuhanga kuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).

Kabla ya uteuzi huo Mhandisi Nyamuhanga alikuwa Katibu Mkuu Ujenzi, na anachukua nafasi ya Mhandisi Mussa Iyombe ambaye amestaafu.

  1. Rais Magufuli amemteua Dkt. Zainabu Chaula kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (anayeshughulikia afya). Kabla ya Uteuzi huo Dkt. Chaula alikuwa Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI (afya).
  2. Rais Magufuli amemteua Arch. Elius Mwakalinga kuwa Katibu Mkuu Ujenzi. Kabla ya uteuzi huo Arch. Mwakalinga alikuwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) na anachukua nafasi ya Mhandisi Nyamuhanga ambaye ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu TAMISEMI.
  3. Rais Magufuli amemteua Bi. Dorothy Mwaluko kuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uwekezaji). Kabla ya Uteuzi huo Bi. Mwaluko alikuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.
  4. Rais Magufuli amemteua Dkt. Dorothy Gwajima kuwa Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI (Afya). Kabla ya uteuzi huo Dkt. Gwajima alikuwa Mkurugenzi wa Tiba wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
  5. Rais Magufuli amemteua Dkt. Francis K. Michael kuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. Kabla ya uteuzi huo Dkt. Francis K. Michael alikuwa Mhandiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
  6. Rais Magufuli amemteua Dkt. Mpoki Ulisubisya kuwa Balozi.

Kabla ya uteuzi huo Dkt. Ulisubisya alikuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (akishughulikia afya). Kituo cha kazi cha Dkt. Ulisubisya kitatangazwa baadaye.

  1. Rais Magufuli amemteua Prof. Faustin Kamuzora kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera.

Kabla ya Uteuzi huo Prof. Kamuzora alikuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera na Uratibu na anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Bw. Athumani Diwani Msuya ambaye ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

Uapisho wa viongozi hao utafanyika kesho tarehe 09 Januari, 2019 saa 3:30 asubuhi, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli ameifuta nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi. Nafasi hiyo ilikuwa inashikiliwa Bi. Immaculate Ngwalle ambaye amestaafu.

Katika hatua nyingine, Mhe. Rais Magufuli amefanya uamuzi wa kufungua Ubalozi Mpya wa Tanzania nchini Cuba. Balozi wa Tanzania nchini Cuba atateuliwa baadaye.

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam

08 Januari, 2019

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi