Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Rais Magufuli Aagiza Kusimaishwa Kazi RPC Kagera na Viongozi wa Polisi Wilaya ya Kyerwa
Oct 09, 2018
Na Msemaji Mkuu

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli leo tarehe 08 Oktoba, 2018 ameagiza kusimamishwa kazi mara moja kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kagera Bw. Augustine Ollomi, Kamanda wa Polisi wa Wilaya ya Kyerwa Bw. Justine Joseph, Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Kyerwa Bw. Everist Kivuyo na Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Kyerwa Bw. Robert Marwa.

Viongozi hao wa Polisi wanasimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za kuhusika katika magendo ya zao la kahawa katika Wilaya ya Kyerwa pamoja na tuhuma nyingine.

Aidha, Mhe. Rais Magufuli amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi Mej. Jen Jacob Kingu na Inspekta Generali wa Polisi Simon Sirro kuhakikisha uchunguzi wa kina unafanyika na hatua stahiki zinachukuliwa endapo watabainika kuhusika katika magendo ya kahawa na makosa mengine kwa mujibu wa sheria.

Tuhuma dhidi ya viongozi wa polisi katika Wilaya ya Kyerwa zimebainika jana wakati wa ziara ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa.

Gerson Msigwa

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU

Dar es Salaam.

08 Oktoba, 2018

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi