Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Rais Dkt. Samia Ana Utashi wa Kukuza Michezo - Majaliwa
Oct 04, 2023
Rais Dkt. Samia Ana Utashi wa Kukuza Michezo - Majaliwa
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia hundi ya shilingi milioni 500 ikiwa ni ahadi ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu, Taifa Stars baada ya kufuzu michuano ya AFCON ya mwaka 2024. Makabidhiano hayo yalifanyika katika uwanja wa Taifa wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salam, Oktoba 4, 2023. Wa pili kushoto ni Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Damas Ndumbaro na kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Albert Chalamila.
Na Ofisi ya Waziri Mkuu

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ana utashi mkubwa wa kisiasa katika kukuza sekta ya michezo kwa kufanya uwekezaji na mabadiliko kwenye sekta hiyo.

 

Amesema hayo leo (Jumatano, Oktoba 4, 2023) wakati wa hafla ya kukabidhi shilingi milioni 500 kwa timu ya Taifa ya mpira wa miguu (Taifa Stars) ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Dkt. Samia kwa timu hiyo baada ya kufuzu michuano ya AFCON 2024.

 

“Uamuzi wa Rais Dkt. Samia wa kuridhia asilimia tano ya kodi itokanayo na michezo ya kubashiri (sports betting) ipelekwe katika Mfuko wa Maendeleo ya Michezo ili kusaidia shughuli za maendeleo ya michezo hapa nchini umelenga kuikuza zaidi sekta hiyo.”

 

Ameongeza kuwa hatua ya Rais Samia kuiundia sekta ya michezo wizara yake ni uthibitisho tosha kwamba anataka kuhakikisha kwamba Tanzania inafikia hatua ambazo mataifa mengine yameshafikia kwenye sekta ya michezo.

 

“Hayo ni baadhi tu ya mambo ya kujivunia katika kipindi hiki cha utawala wa Jemedari na nguli wa michezo, kiongozi shupavu, mama yetu mpendwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.”

 

Kabla ya kukabidhi hundi hiyo, Waziri Mkuu alikagua ukarabati unaoendelea kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa ikiwemo vyumba vya wachezaji kubadilishia nguo, chumba cha matibabu, hali ya uwanja, chumba cha VAR na chumba cha kufuatilia kamera za ulinzi wa uwanjani. Alisema ameridhishwa na kazi ya ukarabati inayoendelea kwenye awamu hiyo ya kwanza.

 

Akimkaribisha Waziri Mkuu, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Damas Ndumbaro alisema kutokana na ahadi ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, vijana wa timu ya Taifa walipambana hadi wakafuzu kwenda AFCON kwa mara ya tatu.

 

Alisema Tanzania, Kenya na Uganda ziliungana na kuomba kuwa wenyeji wa mashindano ya AFCON kwa mwaka 2027. “Nchi hizi tatu, kwa mara ya kwanza zitakutana huko Mombasa mwezi huu wa kumi ili kuratibu shughuli hii kwa pamoja,” alisema.

 

Mapema, Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Nchini (TFF), Wallace Karia alisema mbali na kujenga viwanja vipya huko Arusha na Dodoma, Benjamin Mkapa na Amri Abeid ni miongoni mwa viwanja vinavyofanyiwa ukarabati ili vitumike kufanya mazoezi wakati wa  mashindano ya AFCON.

 

Aliiomba Serikali iwasaidie kupata usafiri wa moja kwa moja kwenda Morocco ili wawahi kurudi nyumbani kwa ajili ya mechi ya marudiano. 

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi