Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Rais Dkt. Samia Aagiza Kuwekwa Mikakati Kuimarisha Usawa kwa Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI
Dec 01, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa kukosekana kwa usawa kwa watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI kunarudisha nyuma juhudi za kutokomeza ugonjwa huu ifikapo mwaka 2030.

Ameyasema hayo leo wakati wa maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani yaliyofanyika katika uwanja wa Ilulu mkoani Lindi ambapo Kauli mbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka huu ni "Imarisha Usawa" ikiwa ni mwendelezo wa kauli mbiu ya mwaka jana ambayo nayo ilijikita katika suala la usawa.

Kaulimbiu hii msisitizo wake ni kuhimiza usawa katika utoaji huduma za kudhibiti VVU na UKIMWI ili kusiwe na maeneo au makundi ya watu yasiyofikiwa na huduma hivyo kuondoa hali ya ubaguzi na unyanyapaa kwa watu wanaoishi na VVU, ni muhimu kutumia maadhimisho haya kutafakari kwa kina na kuhakikisha tunaweka mikakati ya kuimarisha usawa ili lengo la kutokomeza ugonjwa huo litimie, alisema Rais, Dkt. Samia.

Ametoa maagizo mengine kwa Wizara ya Afya, Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) na wadau mbalimbali wa afya kuweka jitihada na mikakati madhubuti katika kuzuia maambukizi mapya ili kuweza kutokomeza kabisa ugonjwa huo, kuimarisha huduma za upimaji wa VVU na matumizi ya ARV ili kutokomeza vifo vitokanavyo na UKIMWI pamoja na kuweka mikakati ya kutokomeza ubaguzi na unayanyapaa kwa wagonjwa wa VVU.

Kwa upande wake Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali inaendelea kufanya jitihada mbalimbali ikiwa ni pamoja na maeneo muhimu matatu ya kimkakati kwenye eneo la UKIMWI huku eneo la kwanza likihusu utafiti wa viashiria vya hali ya VVU na UKIMWI hapa nchini ambapo mwezi Septemba mwaka huu utafiti wa tano wa viashiria vya hali ya VVU na UKIMWI kwa mwaka 2022/23 ulizinduliwa.

“Utafiti huu hufanyika kila baada ya miaka minne na ulianza mwaka 2003/2004, utafiti wa mwaka 2022/2023 utatoa fursa kwa Kaya 19,000 nchini kupima VVU majumbani mwao na kujua hali zao siku hiyo hiyo, alisema Waziri Mkuu, Majaliwa.

Nae Naibu Waziri wa Afya, Mhe. Dkt. Godwin Mollel amesema Tanzania inakadiriwa kuwa na waathirika milioni 1.7 na mpaka sasa wameshawafikia waathirika milioni 1.53. Aidha, inategemewa kufikia mwaka 2026 nchi itimize 95 tatu ambapo 95 ya kwanza ni kuwafikia waathirika, 95 ya pili kuwafikia kuwapa dawa na 95 ya tatu ni kuhakikisha kwamba Virusi vya UKIMWI vimefubazwa.

“Hadi sasa tumeshawafikia asilimia 92.5 ya waathirika wote, vile vile asilimia 98.3 wameshapata dawa na asilimia 97 ni waathirika ambao wamefubaza virusi vya ugonjwa huo, amesema Dkt. Mollel.

Vile vile Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Watu Wanaoishi na Maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (NACOPHA), Bi. Leticia Kapela amemshukuru Rais, Mhe. Dkt. Samia kwa kazin nzuri anayoifanya ya kuleta maendeleo ya Taifa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha watu wanaoishi na Virusi vya UKIMWI wanapata huduma zote ikiwemo kupata dawa za ARV bure.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi