Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ametoa shukrani maalum kwa viongozi na wafanyakazi wa Taasisi ya Benjamin Mkapa kwa ushirikiano wanaoendelea kuutoa kwa Serikali zetu katika kuimarisha huduma mbalimbali hasa za afya.
Rais Dkt. Mwinyi ametoa shukrani hizo leo Zanzibar wakati aliposhiriki Kongamano la pili la kumuenzi Hayati Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Benjamin Mkapa.
Rais Dkt. Mwinyi amefafanua kuwa, kwa upande wa Zanzibar taasisi hiyo imeshirikiana na Wizara ya Afya katika kuimarisha mifumo ya utoaji wa huduma, mafunzo na katika kutekeleza mipango itakayotuwezesha kuanzisha Bima ya Afya.
“Ni vyema Asasi nyingine za kiraia zikaiga mfano huu kwani ushirikiano mzuri uliopo baina ya Serikali na Sekta Binafsi unasaidia sana katika juhudi zetu za kupambana na maradhi ikiwemo ya UVIKO 19”, alisema Rais Dkt. Mwinyi.
Amesisitiza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweka kipaumbele cha kuimarisha ushirikiano na Sekta Binafsi pamoja na Asasi za Kiraia.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Benjamin Mkapa, Dkt. Ellen Senkoro ameishkuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuonesha dhamira ya dhati ya kuishirikisha Sekta Binafsi katika ajenda zote za maendeleo.
Akiongelea kuhusu kumbukizi ya Hayati Benjamin Mkapa, amesema kuwa walianzisha kumbukizi za kila mwaka za Hayati Mhe. Mkapa ili waweze kusheherekea maisha yake na kuamua kuanzisha Mfuko wa kuendeleza shughuli za Benjamin Mkapa ili kuweza kuendeleza hadi kwenye vizazi vijavyo.
“Hayati Mhe. Benjamin Mkapa alituambia kuhusu uongozi himilivu ambapo yeye mwenyewe ni mfano wa uongozi huo, akiwa ofisini aliendeleza mabadiliko mbalimbali ya kiuchumi na uongozi wa umma ambayo yalibadilisha nchi yetu kutoka kwenye uchumi uliofungwa mpaka kwenye uchumi uliofunguka”, alimalizia Dkt. Senkoro.