Na Lilian Lundo na Beatrice Lyimo- MAELEZO, DODOMA
Rais Dkt. John Pombe Magufuli amesamehe jumla ya wafungwa 8,157 katika maadhimisho ya miaka 56 ya Uhuru wa Tanzania Bara yaliyofanyika leo katika uwanja wa Jamhuri, Mjini Dodoma.
Msamaha huo umehusisha wafungwa 1828 ambao watatolewa kaunzia leo na wengine 6329 wamepunguziwa muda wa vifungo vyao, aidha kati ya wafungwa watakaoachiwa huru wafungwa 61 ni wafungwa ambao walihukumiwa kunyongwa.
“Kuna wafungwa ambao wamehukumiwa kunyongwa wana umri wa miaka 85 na wapo waliokaa gerezani zaidi miaka ya miaka 45, ambao wametubu na kukiri makosa na wapo ambao hawakuwauwa maalbino wala hawakuwa majambazi,” amesema Dkt. Magufuli.
Dkt. Magufuli ametoa mfano wa mfungwa anayejulikana kama Mganga Matonya mwenye umri wa miaka 85 yupo kwenye orodha ya wafungwa watakaoachiwa huru leo ambapo amekaa gerezani kwa miaka 37 na mahabusu miaka saba (7) kabla hajahukumiwa.
Katika hatua hiyo, Rais Dkt. Magufuli amewaachia huru Nguza Viking na Johson Nguza (Papii Kocha) waliohukumiwa kifungo cha maisha.
Aidha Mhe. Rais amesema kuwa msamaha huo alioutoa leo umetokana na mamlaka aliyonayo kutoka kwenye Ibara ya 45 (a) (b) (c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayomruhusu Mhe. Rais kutoa msamaha, kumuachia huru, kubadilisha adhabu au kufuta adhabu kwa mtu yoyote aliyehukumiwa kwa kosa lolote.
Wakati huo huo, Rais Magufuli ametoa wito kwa watanzania wote kuenzi na kudumisha tunu na amani zilizoachwa na waasisi wa Taifa.
Aidha, Rais Magufuli ameeleza kuwa tangu nchi ipate uhuru kumekuwa na maendeleo katika nyanza mbalimbali ikiwemo barabara, madaraja, vituo vya afya, shule za msingi na shule za sekondari.
“Wakati nchi inapata uhuru kulikuwa na jumla ya kilometa 32,600 za barabara ambapo kilometa 1360 zilikuwa katika kiwango cha lami, lakini mpaka sasa nchi inapotimiza miaka 56 ya uhuru kuna jumla ya kilometa 122,500 za barabara ambapo kati ya hizo kilometa 12,679.55 zipo katika kiwango cha lami, kilometa 2,480 zinaendelea kujengwa katika kiwango cha lami na kilometa 7087 zipo kwenye hatua mbalimbali za maandalizi za kujengwa katika kiwango cha lami” anasema Rais Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli amesema kuwa, Mfalme wa Morroco amemtuma Spika wa nchi hiyo kuja kuangalia eneo litakalojengwa uwanja mkubwa wa Kimataifa Mkoa wa Dodoma ambapo unatarajiwa kuwekwa jiwe la msingi mwezi Machi au Aprili mwaka 2018.
Mbali na hayo Sherehe hizo zilipambwa na gwaride kutoka Majeshi ya Tanzania, onesho la kikundi cha Komando, onesho la gwaride la Uzalendo la wanafunzi, vikundi mbalimbali vya kwaya, ngoma za alisi na Tanzania Allstars.
Mwisho….