Na: Lilian Lundo - MAELEZO, Dodoma.
Mkoa wa Pwani unatekeleza jumla ya miradi 141 ya Maji kupitia bajeti ya Serikali ambayo inatorajiwa kukamilika katika mwaka wa fedha 2017/2018.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Mkoa huo Mhandisi Evarist Ndikilo alipokuwa akitoa tathimini ya utendaji ya Mkoa wa Pwani katika kipindi cha Tunatekeleza kinachoratibiwa na Idara ya Habari (MAELEZO) na kurushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).
"Tunachimba zaidi ya visima 600 virefu na 900 vifupi katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Pwani. Dhumuni ni kuongeza hali ya upatikanaji wa maji mkoani humu ili kumtua mama ndoo kichwani," alisema Mhandisi Ndikilo.
Wakati huo huo Mhandisi Ndikilo amesema, Mkoa huo una viwanda 398 vinavyofanya kazi na bado mkoa unaendelea na jitihada za kuongeza idadi ya viwanda ambapo mkoa umetenga jumla ya ekari 1500 kwa ajili ya ujenzi wa viwanda mbalimbali.
"Asilimia kubwa ya viwanda vilivyopo mkoani wa Pwani vinatumia malighafi zinapatikana hapahapa Mkoani, japo kuna baadhi tunatoa nje ya Mkoa," alisisitiza Mhandisi Ndikilo.
Aidha amesema, ongezeko kubwa la viwanda mkoani humo umesaidia kuongeza ajira kwa wakazi wa Mkoa wa Pwani na wale wanaotoka nje ya Mkoa huo .
Kwa upande wa Afya, Mhandisi Ndakilo amesema hali ya upatikanaji wa dawa katika Hosipitali, Vituo vya Afya na Zahanati mkoani humo ni nzuri, Hatua nyingine zilizochukuliwa ni ukarabati na kuviongezea bajeti vituo vya afya ili viweze kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za afya.
Vile vile mkoa huo upo katika hatua za mwisho za ukamilishaji wa kituo cha mabasi ya kisasa chenye uwezo wa kuegesha mabasi makubwa 60 na mabasi madogo 60 ambacho kinatarajiwa kuzinduliwa mwezi Agosti mwaka huu.
Kipindi cha Tunatekeleza kinarushwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na awamu hii inawashirikisha Wakuu wa Mikoa yote Tanzania Bara, Kipindi hiki kimekuwa fursa kwa watendaji wa Serikali kuwasiliana na wananchi kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo na program mbalimbali zinazolenga kuwaletea wananchi maendeleo.