Na. Georgina Misama – MAELEZO
Serikali imepitia na kufanya marekebisho ya Tozo mbalimbali ambazo utekelezaji wake unatarajiwa kuanza Oktoba 1, 2022 zikiwemo za kuhamisha fedha kutoka Benki kwenda mitandao ya simu, kuhamisha fedha ndani ya Benki moja, kuhamisha fedha kutoka Benki moja kwenda nyingine pamoja na msamaha wa tozo za miamala kwenye utoaji wa fedha taslimu kupitia Wakala wa Benki na ATM.
Akitoa ufafanuzi huo leo Bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu amesema punguzo la tozo hizo litapunguza mapato ya Serikali na kuelekeza fedha hizo zifidiwe kutokana na kubana matumizi mengineyo ndani ya Serikali ambayo hayataathiri utekelezaji wa majukumu ya msingi ya mafungu husika.
“ Namwelekeza Mlipaji Mkuu wa Serikali kukaa na Maafisa Masuuli wote kuyaangalia upya mafungu ya matumizi mengineyo ili miradi ya maendeleo isiathirike kwa hatua hii, tupunguze kwenye chai, vitafunwa, misafara pamoja na safari za ndani na nje kwa Maafisa wa Wizara zetu kama Rais, Mhe. Samia Suluhu Hassan alivyoelekeza tukate mafunzo, semina, matamasha, warsha na matumizi ya mafuta,” alisema Dkt. Mwigulu.
Sambamba na hatua hiyo, Dkt Mwigulu alisema Serikali inafuta utaratibu wa kodi ya zuio inayotokana na pango kukusanywa na mpangaji na badala yake jukumu hilo linarejeshwa kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kama ilivyokuwa awali kwa utaratibu utakao bainishwa kwenye Kanuni.
“Napenda kusisitiza kuwa kodi ya zuio ya pango siyo ya mpangaji bali inapaswa kulipwa na mpangishaji ambaye ndiye anapokea mapato kutokana na uwekezaji au biashara ya kupangisha, utaratibu huo umekuwa ukitumika kwa muda mrefu kwenye nyumba za biashara na nyumba zinazopangishwa kwenye makampuni au mashirika yanayofunga ritani za kodi,” alihitimisha Dkt. Mwigulu.