Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

PSSSF Wapata Faida ya Bilioni 581.72 katika Uwekezaji
Nov 09, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO

Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) umepata jumla ya Shilingi bilioni 581.72 kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni, 2022 ikiwa ni faida ya uwekezaji mbalimbali unaofanywa na Mfuko huo.

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo, CPA. Hosea Kashimba ametaja faida za uwekezaji wa taasisi hiyo leo Jijini Dodoma wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Mfuko na Mwelekeo wa Utekelezaji kwa mwaka 2022/23.

CPA. Kashimba amesema, uwekezaji ni moja ya majukumu makuu ya kisheria ya Mfuko huo ambapo malengo ya uwekezaji ni kulinda thamani ya fedha za wanachama dhidi ya mfumuko wa bei na kushuka kwa thamani ya fedha, kukuza hazina na kuongeza uwezo wa kulipa mafao pale yanapoiva na kuwezesha Mfuko kuwa na uendelevu.

“Hadi kufikia mwezi Juni 2022, Mfuko ulikuwa na uwekezaji wenye thamani ya Shilingi trilioni 7.5 na tumewekeza katika maeneo mbalimbali yakiwemo ya hatifungani za Serikali, majengo ya biashara, uwekezaji wa viwanda, hisa za makampuni, amana za mabenki na mifuko ya uwekezaji wa pamoja, uwekezaji huu umeleta faida ya jumla ya Shilingi bilioni 581.72", alisema Mkurugenzi Kashimba.

Mkurugenzi Kashimba amefafanua mgawanyo wa uwekezaji huo ambapo hatifungani za serikali ni 60%, majengo ya biashara 16%, hisa za makampuni 11%, amana za mabenki 5%, mifuko ya uwekezaji wa pamoja ni 4% na maeneo mengine ya uwekezaji ni 4% ambapo kutokana na uwekezaji huo, Mfuko hupata faida ya uwekezaji wa wastani wa asilimia 8 kwa mwaka, ambayo ni juu ya Mfumuko wa bei na hivyo kufanya uwekezaji huo kuwa na tija.

Vilevile, Mfuko umewekeza katika miradi minne ya viwanda ambayo ni Ranchi ya Mifugo na Machinjio ya Kisasa ya Nguru Hills, Kiwanda cha kusindika chai, Kiwanda cha bidhaa za ngozi na Kiwanda cha kuchakata tangawizi ambapo uwekezaji katika viwanda unatarajia kuongeza wigo wa uwekezaji wa muda mrefu unaowiana na jukumu la Mfuko la kulipa mafao ya muda mrefu, kuongeza mapato ya uwekezaji na kuongeza wanachama wa Mfuko kupitia ajira zitakazozalishwa.

Aidha, hadi kufikia mwezi juni 2022 Mfuko ulikuwa umeshawekeza kiasi cha Shilingi bilioni 130 katika miradi ya viwanda ambapo miradi hiyo ipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi