Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Programu ya Kuelimisha Wateja Yazinduliwa Mahakama Kuu Kanda ya Dar Es Salaam
Aug 29, 2018
Na Msemaji Mkuu

Na Mary Gwera

Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam imezindua rasmi programu maalum ya kuzungumza na wateja wake kwa lengo la kutoa elimu kuhusu taratibu mbalimbali za Kimahakama na vilevile kuongeza uwazi katika utoaji wa huduma zake.

Akizindua rasmi zoezi hilo mapema Agosti 29, kwa niaba ya Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu- Kanda ya Dar es Salaam; Jaji wa Mahakama Kuu-Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Ilvin Mugeta alisema kuwa zoezi hili ni miongoni mwa maboresho ya Mahakama ikiwa ni mkakati wa kuwafikia wananchi kwa karibu zaidi.

Katika maneno yake ya ufunguzi, Mhe. Jaji Mugeta alisema kuwa zoezi hilo litakuwa likifanyika mara moja kwa juma, ambayo ni Jumatano ya kila wiki kuanzia saa 02:00 asubuhi hadi saa 02:15 asubuhi.

“Sisi Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, tumeona ni vyema tukawa na muda mfupi angalau mara moja kwa wiki kuzungumza na wateja wetu na Umma wote kwa ujumla kuhusu huduma zetu,” alisema Jaji Mugeta.

Kwa upande wake, Naibu Msajili Mfawidhi, Mahakama Kuu-Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Joachim Tiganga alisema kuwa lengo la kampeni hiyo si tu kutoa elimu bali pia kupokea changamoto mbalimbali kutoka kwa wateja kwa lengo la kujiboresha zaidi katika utoaji wa huduma zake.

Mhe. Tiganga alitoa wito kwa wananchi kutosita kutoa malalamiko yao kwa Watumishi wa Kanda hiyo ikiwemo Manaibu Wasajili na Makarani ili waweze kupatiwa ufumbuzi.

Aidha; mbali na kuwaona Wasajili na Makarani wa Kanda hiyo, Mhe. Tiganga aliwataka wananchi pia kutuma Malalamiko yao kwa njia ya ujumbe mfupi wa maandishi kupitia simu nambari 0735 501 400.

Nao baadhi ya Wananchi walioshiriki katika uzinduzi huo waliipongeza Mahakama kwa uamuzi huo kwani itawasaidia kujua zaidi taratibu mbalimbali za Mahakama na kuondoa baadhi ya maswali waliokuwa wakijiuliza.

Bw. Rajab Mwimi na Bi.Hamisa Chaurembo ni miongoni mwa wananchi walioshiriki katika zoezi hilo, ambapo waliipongeza Mahakama Kanda ya Dar es Salaam kwa kuanzisha huduma hiyo ambayo itawarahisishia katika kutafuta huduma ya haki zao.

“Zoezi hili nimelipokea vizuri na nimelipenda, tunaishukuru Mahakama kwa kusikiliza kero za wananchi na kutuelimisha, vilevile naiomba iendelee kusukuma mashauri haraka na haki zitendeke bila upendeleo,” alieleza Bi. Chaurembo.

Zoezi la utoaji elimu kwa wananchi na kuwasikiliza wateja wanaofika katika Mahakama nchini tayari limeshaanza katika Kanda mbalimbali za Mahakama, ikiwa ni pamoja na Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Tabora, Dodoma na kadhalika.

Mahakama ya Tanzania kupitia Mpango Mkakati wake imejiwekea nguzo kuu tatu moja ya nguzo hizo ni ya Kurejesha imani ya jamii na Ushirikishwaji wa Wadau ambapo kupitia nguzo hii Mahakama inafanya jitihada mbalimbali  ili wananchi waweze kujua zaidi huduma na maboresho yanayojiri kwa manufaa ya wananchi kwa kuwa wao ndio wadau wakubwa wa Mhimili huu.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi