Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Prof. Olesante Ataka Mageuzi ya Kifikra kwa Watanzania Kuhusu Mahakama
Aug 31, 2021
Na Jacquiline Mrisho

Na Mwandishi Wetu

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel amewataka Watanzania kubadilisha fikra zao kuhusu utendaji wa Mahakama kwa kuwa inaanza kutumia mifumo ya kisasa itakayorahisisha mnyororo wa utoaji haki kwa wananchi.

Prof. Elisante ameyasema hayo leo jijini Dodoma wakati alipofanya ziara ya kukagua jengo la Mahakama Kuu ya Tanzania pamoja na Kituo Jumuishi cha utoaji haki yanayoendelea kujengwa jijini hapo.

 “Inaweza kuchukua muda kwa Watanzania kuamini na kuzoea kwamba wanaweza kufungua kesi hata wakiwa nyumbani, unajua watu wakishazoea kuwa lazima wachelewe chelewe ama watoe rushwa inakuwa changamoto kubadilika, sasa kupitia mifumo hata Karani tu hutamuona. Hivyo, wakati umefika kwa Watanzania kubadilisha fikra zetu kuhusu Mahakama”. Alisema Prof. Elisante.

Ameongeza kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuweka mkazo wa kipekee katika kuhakikisha kwamba haki inapatikana kwa haraka na usahihi pamoja na kuhakikisha kwamba mazingira na masilahi ya Watumishi wa Mahakama yanaboreshwa.

Kwa upande wake Mkuu wa kitengo cha Usimamizi wa Majengo cha Mahakama, Khamudu Kitunzi amesema kuwa majengo hayo yamewekewa mifumo ya TEHAMA inayomuwezesha mwananchi kufungua kesi kwa njia ya mtandao na kuweza kufuatilia kuanzia shauri linapofunguliwa mpaka mwisho wa kesi.

“Tumetengeneza vigezo vya upimaji wa Kituo Jumuishi cha utoaji haki tofauti na Mahakama zingine, kwa Mahakama ya Mwanzo tumepunguza muda wa kusikiliza mashauri kutoka miezi sita hadi siku 30, kwa Mahakama za Wilaya na Hakimu Mkazi tumepunguza muda kutoka miezi 12 hadi siku 45 na Mahakama Kuu kutoka miezi 24 hadi miezi sita”, alisema Kitunzi.

Msanifu Majengo kutoka Kampuni ya Arques Africa inayoshauri, kusanifu na kusimamia jengo la Mahakama Kuu, Rosemary Nestory amesema kuwa jengo hilo limezingatia watu wenye mahitaji maalum kwa kuwawekea njia pamoja na vyoo vyao.

Pia, jengo hilo lina mfumo wa umeme wa jua utakaosaidia kupunguza gharama za Serikali za uendeshaji wa ofisi hiyo.   

Mpaka sasa Tanzania ina Mahakama za Mwanzo 960, Mahakama ya Wilaya 119, Mahakama za Hakimu Mkazi 29, Mahakama Kuu 17 na Mahakama ya Rufani moja, Mahakama Kuu ya Tanzania inayojengwa jijini Dodoma itagharimu zaidi ya Bilioni 120.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi