Wadau wa Shirika la Mawasiliano Duniani (ITU) wanaohusika na masuala ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) wamekutana Tanzania kutoka nchi mbali mbali duniani kwenye Mkutano wa Nane wa Wiki ya Kijani kwa lengo la kujadiliana namna ya kutumia TEHAMA kuendana na mabadiliko ya tabia nchi yanaoendelea kutokea duniani.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Prof. Makame Mbarawa amefungua mkutano huo uliofanyika Zanzibar ambao umeandaliwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) na Mamlaka ya Mawasiiano Tanzania (TCRA) wakiwa waandaji na wenyeji wa mkutano huo.
Wakati akifungua mkutano huo, Prof. Mbarawa amewataka wataalamu wote wa TEHAMA kutoka sehemu mbali mbali duniani kutumia mkutano huo kujadiliana, kuweka mikakati na miongozo ya namna ya kutumia huduma na bidhaa za TEHAMA kwa maendeleo ya uchumi na viwanda ikiwa ni pamoja na mbinu za kutabiri na kudhibiti majanga yanayotokea kuendana na mabadiliko ya tabia nchi kwa kutumia TEHAMA.
Amewataka washiriki wa mkutano huo kubadilishana uzoefu na kujadiliana namna ya kutumia TEHAMA kulinda mazingira, kufungua fursa za kiuchumi, kuwa na miji ya kisasa ambayo inaendeshwa na kusimamiwa kwa kutumia TEHAMA illi kuhakikisha kuwa TEHAMA inatumika kutunza mazingira ili kupunguza uchafuzi wa mazingira kutokana na mabaki ya vifaa na huduma za TEHAMA na kuweza kurudufu mabaki hayo ii kulinda usalama wa mazingira na yaweze kutumika kwa matumizi mengine.
Amefafanua kuwa Tanzania imejenga Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano wenye urefu wa zaidi ya kilomita 25,000 ambao umeunganishwa kwenye taasisi za Serikali na sekta binafsi na kwenye nchi za jirani ambazo hazijapakana na bahari ambapo umewezeshaji utoaji wa huduma za mawasiliano nchini ambapo hadi hivi sasa tuna jumla ya watanzania milioni 45 wanaotumia simu za mkononi, milioni 23 wanaopata huduma ya intaneti na milioni 20 wanaotumia huduma za kielektoniki kama vile kutuma na kupokea pesa, “watu hao wote wanatumia vifaa mbalimbali vya kielektroniki, baada ya muda vifaa hivi vitakuwa havifanyi kazi, vimepitwa na wakati, sasa inatakiwa tuvitoe kwenye soko vizuri bila kuharibu mazingira ambayo tunayatumia, sasa tukikaa hapa na wataalamu hawa tunaamini tutajifunza njia mbali mbali ambazo zinatumika duniani katika kuharibu hivi vifaa vya kielektroniki ambavyo vimeshapitwa muda wake” amesema Prof. Mbarawa.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano na Viwango wa Shirika la Mawasiliano Duniani (ITU) Dkt. Chaesub Lee amewataka wataalamu hao kujadiliana na kupeana uzoefu wa kutoka kwenye nchi zao za kutumia fursa za TEHAMA kuongeza mzunguko wa uchumi na viwanda duniani, kutumia bidhaa na huduma za TEHAMA kuhifadhi na kulinda mazingira na kuchakata bidhaa na huduma za mawasiliano ambazo zimepitwa na muda wake au kuharibika ambapo ITU iko tayari kushirikiana na nchi husika katika nyanja ya utalaamu, ushauri na utekelezaji wa mipango na mikakati mbalimbali ya namna ya kutumia TEHAMA kuendana na mabadiliko ya tabia nchi kulingana na mahitaji ya nchi husika.
Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dkt. Sira Ubwa Mwamboya wakati akifunga mkutano huo, amewakaribisha washiriki hao kutembelea vivutio mbali mbali vya kiutalii vilivyopo kwenye visiwa hivyo.
Mkutano huo umeandaliwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania kwa niaba ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano