Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel akifungua mkutano wa kujadili utekelezaji wa Programu ya Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika kati ya Tanzania na Afrika Kusini leo mjini Dodoma.
Na Beatrice Lyimo - MAELEZO, DODOMA
Watanzania wametakiwa kutunza, kulinda na kuimarisha amani na heshima iliyopo nchini kwani amani hiyo huifanya Tanzania iheshimike na Mataifa mengine.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel wakati akifungua mkutano wa kujadili utekelezaji wa Programu ya Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika kati ya Tanzania na Afrika Kusini unaofanyika mjini Dodoma.
Prof. Elisante amesema kuwa suala la kutunza na kulinda amani iliyopo huanzia kwa wananchi wenyewe, hivyo ili Tanzania iendelee kuheshimika haina budi kutunza na kulinda heshima na utamaduni uliopo kwani amani na heshima vikitoweka huchukua muda mrefu kuijenga au kuirejesha.
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel akiongea na Waandishi wa Habari mara baada ya kufungua mkutano wa kujadili utekelezaji wa Programu ya Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika kati ya Tanzania na Afrika Kusini leo mjini Dodoma.
“Tanzania imeendelea kuheshimika na kuimarika kutokana na amani na utulivu uliopo, hivyo sisi kama Watanzania tunahitaji kuitunza, kuheshimu na kuimarisha amani iliyopo kwani suala la heshima huanzia ndani”, aliongeza Profesa Elisante.
Akizungumzia mkutano huo, Prof. Elisante amesema kuwa unalenga kuwa na mazungumzo kati ya nchi mbili za Tanzania na Afrika Kusini kabla ya kuelekea Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), hatua hiyo inatokana na Afrika Kusini kuwa na maudhui ya kipekee ya jinsi Tanzania ilivyoshiriki katika ukombozi wa Bara la Afrika ikiwemo Afrika Kusini.
Prof. Elisante ameongeza kuwa lengo lingine la mkutano huo ni kuweka historia ili kizazi kijacho kitambue ushiriki wa Tanzania katika ukombozi wa bara la Afrika ikiwemo Afrika Kusini.
Mwenyekiti wa Mkutano, Balozi Christopher Celestine Liundi akitoa utaratibu utakaotumika wakati wa mkutano wa wataalamu kutoka Tanzania na Afrika Kusini wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kujadili utekelezaji wa Programu ya Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika leo mjini Dodoma.
Aidha, lengo la Programu hiyo ni kutambua umuhimu wa Vyama vya Ukombozi katika harakati za kulikomboa Bara la Afrika na kuthamini mchango mkubwa uliotolewa na Tanzania katika kusaidia kwa hali na mali harakati za ukombozi wa Bara la Afrika.
Zaidi ya hayo, Prof Elisante amesema kuwa Tanzania imefaidika katika nyanja mbalimbali zikiwemo kisiasa, Kiuchumi na Kiutamaduni ambapo kisiasa Tanzania imeendelea kuheshimika ndani na nje ya Bara la Afrika hatua inayopelekea kuongeza pato la Taifa kutokana na utalii unaofanyika katika maeneo ya kihistoria yaliyotumika wakati wa harakati za Ukombozi wa Bara la Afrika.
Kwa upande wake Mkurungenzi Mkuu wa Kazi za Umma kutoka Afrika Kusini Bw. Mziwonke Dlabantu amesema kuwa timu hizo zimekutana kuimarisha uhusiano uliopo kati ya Tanzania na Afrika Kusini ili kujadiliaana na kuimarisha namna bora ya kutekeleza Mradi wa Ukombozi wa Bara la Afrika pamoja na kutembelea baadhi ya maeneo yaliyotumika wakati wa Ukombozi wa Bara la Afrika ikiwemo Afrika Kusini.
Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof. Elisante Ole Gabriel akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa mkutano wa kujadili utekelezaji wa Programu ya Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika kati ya Tanzania na Afrika Kusini leo mjini Dodoma.
Wadau wanaoshiriki mkutano huo kutoka Tanzania na Afrika Kusini ni wizara na taasisi mbalimbali kutoka pande zote mbili ikiwemo Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambao ndio waratibu wa program hiyo, Wizara Fedha, Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Maliasili na Utalii, Ulinzi, Elimu, Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Utalii, Habari na Utamaduni kutoka Zanzibar pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu Sayansi na Utamaduni (UNESCO).
Programu hiyo ina wajibu wa kukusanya, kuweka kumbukumbu, kuhifadhi na kukumbuka nakishi ya Urithi wa Afrika tangu harakati za kupigania Uhuru wa Afrika hadi Bara zima lilipokombolewa.
Mkutano huo unafanyika mjini Dodoma kwa muda wa siku tatu ambapo umegawanyika katika makundi matatu ukihusisha Wataalamu wa Programu, Makatibu Wakuu kutoka katika Wizara zinazohusika katika utekelezaji wa program hiyo pamoja na Mawaziri husika katika Wizara hizo.