Na Mwandishi Wetu - HESLB
Mwenyekiti Mpya wa Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, Prof. Khamis Dihenga ameongoza kikao chake cha kwanza cha Wajumbe wa Bodi hiyo baada ya kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan hivi karibuni.
Kikao hicho kilifanyika jana (Jumatano Februari 9, 2022) ili kupokea na kujadili taarifa za utendaji kazi za HESLB kwa nusu mwaka wa 2021/2022.
Pamoja na mambo mengine, Prof. Dihenga ameipongeza Menejimenti ya HESLB kwa kuendelea kuongeza ufanisi na kuahidi ushirikiano ili kuboresha zaidi utendaji kazi.
“Ukiona kuna utulivu ujue kuna kazi kubwa inafanyika nanyi pamoja na wadau wengine na unaona katika taarifa zenu, hivyo nawapongeza sana”, amesema Prof. Dihenga ambaye pia ni Katibu Mkuu mstaafu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Akiongea baada ya kikao hicho, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB ambaye pia ni Katibu wa Bodi ya Wakurugenzi, Abdul-Razaq Badru amesema ajenda kubwa ya HESLB kwa sasa ni kufanya mapitio makubwa ya mfumo wa sasa wa ugaharamiaji wa elimu ya juu ili kuakisi maoni ya wadau na hali ya sasa.
“Tunafanya mapitio makubwa mwaka huu ya utaratibu wa sasa wa mikopo ya elimu ya juu ili kuwa na mfumo unaoakisi hali ya sasa na maoni ya wadau wetu ambao ni wabunge, wanafunzi, waajiri, wazazi, mamlaka za ithibati na taasisi za elimu ya juu”, amesema Badru.
Aidha katika kikao hicho, Badru alimkabidhi Prof. Dihenga tuzo ya ushindi wa nafasi ya tatu kwa taasisi za umma zinazotumia mwongozo wa wa viwango vya kimataifa wa hesabu za umma “IPSAS” katika uandaaji wa hesabu kwa mwaka 2020 iliyotolewa kwa HESLB na Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA).
Bodi ya Wakurugenzi ya HESLB ina jumla ya wajumbe tisa ambao ni Prof. Charles Kihampa, Dkt. Adolf Rutayuga, Dkt. Ernest Mwasalwiba, Idd Khamis Haji, Haruni Matagane, Theresia Henjewele, Salama Makame (Makamu Mwenyekiti) na Tenelife Mwatebela.