Prisca Ulomi na Loema Joseph, Dodoma
Serikali imelitaka Shirika la Posta Tanzania (TPC) kutumia mfumo wa anwani za makazi na postikodi kubuni huduma mpya kwa wateja ili utekelezaji wa mfumo huo utakapokamilika uweze kutumika ipasavyo kufikisha huduma na bidhaa kwa wateja
Hayo yameelezwa na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Teddy Njau wakati akifungua semina ya mafunzo ya kujenga uelewa kuhusu mfumo wa anwani za makazi na postikodi kwa Mameneja wa Mikoa ya Shirika hilo wa Tanzania Bara na Zanzibar
Njau amewataka washiriki hao kuweka anwani za makazi kwenye maeneo yao, kwa wateja wao na kubuni huduma mpya zitakazotumiwa na wateja kupitia mfumo wa anwani za makazi utakapokamilika utekelezaji wake kwa kuwa Shirika hilo lina mtandao mpana nchi zima na ni wadau wa msingi wanaotakiwa kutumia miundombinu hiyo
“Kila mmoja wetu ana jukumu la kuhakikisha anwani za makazi zinawekwa na kutumika nchi nzima, leo mnapatiwa mafunzo ya kujenga uelewa ili mkasimamie na kushiriki utekelezaji wa mfumo huu kwenye mikoa yenu Tanzania Bara na Zanzibar kwa kuwa ninyi ni wadau muhimu na ni wajumbe kwenye kamati za kitaalam,” amesisitiza Njau
Akizungumza kabla ya kumkaribisha Mgeni Rasmi kufungua mafunzo hayo, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mawasiliano wa Wizara hiyo, Caroline Kanuti amesema kuwa mfumo wa anwani za makazi utakuwa wa kidijitali ili kutoa fursa kwa Serikali kutekeleza majukumu ya sensa ya watu na makazi ili anwani zijumuishwe kwenye sensa inayoanza mwezi Agosti mwaka huu
Ameongeza kuwa utekelezaji wa mfumo wa anwani za makazi utafanyika kwa miezi mitano nchi nzima kwenye kata na wadi 4,174; halmashauri 196 na mikoa 31 ili zoezi hili likamilike ipasavyo na taarifa zake ziwekwe kwenye tovuti maalum na zitumike kwenye simu za mkononi ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi
Naye Kaimu Postamasta Mkuu wa Shirika hilo, Macrice Mbodo amesema kuwa Shirika lake ni mdau muhimu katika anwani za makazi na postikodi ndani na nje ya nchi kwa kuwa posta zote duniani zina jukumu la kutoa anwani zinazotambulika na muundombinu huu utakapokamilika Shirika litatumia anwani za makazi kusafirisha huduma na bidhaa kwa wananchi mpaka nyumbani kwa kuwa tayari tuna duka mtandao
“Mwananchi anaweza kununua na kuuza huduma au bidhaa na kuweka anwani yake kisha atasafirishiwa mzigo wake mpaka mahali alipo na mwananchi atatumia muda wake kutekeleza majukumu mengine ya kiuchumi na kijamii badala ya kufuata mzigo wake, tutashirikiana na viongozi na wataalam wengine nchi nzima kutekeleza hili,” amesema Mbodo
Amesititiza kuwa Shirika lina duka mtandao ambalo linamuwezesha mwananchi wa ndani na nje ya nchi kufanya biashara mtandao na kutumia huduma za Shirika hilo kwa kuwa limeunganishwa na mtandao wa ofisi nyingine za Posta 670 duniani zilizopo kwenye nchi 192 wanachama wa Umoja wa Posta Duniani (UPU) ambapo Tanzania ni nchi mwanachama