Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Geophrey Pinda amesitisha mpango wa Halmashauri ya Wilaya ya Same kuchukua eneo la wananchi wa kijiji cha Makanya lenye ukubwa wa Ekari 4,000 lililotengwa kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda bila kushirikisha wananchi hao kwa madai kuwa ni wawekezaji.
Pinda ametoa kauli hiyo leo Agosti 17, 2023 wilayani Same mkoani Kilimanjaro, wakati wa kikao na viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Same na kubaini mpango huo wa Watumishi wa Umma kujigeuza wawekezaji katika eneo hilo kwa kujimilikisha kwa gharama zisizokuwa na tija.
“Kitu cha ajabu ni kwamba Watumishi wa Umma mmegawana ekari 4,000 kwa kupangisha kila mmoja ekari 25 kwa malipo ya shilingi milioni moja tu kwa kipindi cha miaka 20 hadi 25, yaani kiasi hiki cha fedha kwa watumishi mnaojiita wawekezaji hakina tija yoyote kwa Taifa,” amesema Naibu Waziri Pinda.
Amesema mpango huo wa watumishi wa Serikali kujimilikisha eneo lililotengwa kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda na badala yake kulifanya kuwa la kilimo bila makubaliano ya wananchi huku watumishi wa umma kujigeuza wawekezaji jambo ambalo lilipingwa na wananchi wa eneo hilo.
“Nashangaa sana kuona watumishi wa Serikali ndio mnataka kuwa chanzo cha mgogoro wa ardhi kwa kitendo cha kulibadilishia mpango wa matumizi ya ardhi ya uwekezaji kuwa ya kilimo cha vitalu vya katani kitendo ambacho kilipingwa na wananchi sababu walitenga eneo jingine ambalo lingeweza kutumiwa kwa ajili ya kilimo,” aliongeza Mhe. Pinda
Amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Same, Kasilda Mgeni kuhakikisha anafuatilia kwanini Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Same amebariki mpango huu mbovu ambao hauna masilahi kwa wananchi na hata halmashauri yenyewe kujinyima mapato.
Vilevile amemuelekeza Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Anastazia Tutuba kuhakikisha eneo lingine lililotengwa kwa ajili ya michezo lirudishwe kwenye matumizi yake halisi kwani Halmashauri ya Wilaya ya Same ilibadilisha matumizi ya eneo hilo na kulifanya kuwa eneo la mnada.