Nchi wanachama za Umoja wa Posta Afrika (PAPU) zakubaliana kuwa na mifumo ya kidijitali ya kutoa huduma za posta katika nchi zao.
Akizungumza leo jijini Arusha wakati akifungua Mkutano wa 41 wa Baraza la Utawala la Umoja wa Posta Afrika, Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Mhandisi Kundo Mathew amesema kuwa nchi wanachama wa Umoja wa Posta Afrika umefikia uamuzi huo ili kuwa na kiwango sawa cha utoaji huduma za posta kwa mfumo wa kidijitali.
“Wanachama wa Umoja wa Posta Afrika sasa hawataki kuachana kwamba pengine Nigeria, Kenya au Uganda wako hatua fulani, na ndio umuhimu sasa wa vikao kama hivi tunataka tutembee pamoja kama Afrika”, ameeleza Mhe. Kundo.
Amefafanua kuwa Nchi Wanachama wa PAPU wanaingia katika mifumo ya kidijitali kwa kuweka miundombinu itakayowezesha matumizi mazuri ya huduma za kidijitali.
Aidha, Mhe. Kundo ameongeza kuwa katika jengo la makao Makuu ya Umoja wa Posta Afrika litakalozinduliwa jijini Arusha na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan mnano tarehe 2 Septemba, 2023 litakuwa na ofisi maalumu itakayotumika katika kuwajengea uwezo wataalam wa posta kutoka Nchi wanachama ili kufikia kiwango kimoja cha utoaji huduma za posta kwa wateja.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Umoja wa Posta Duniani (UPU), Bw. Mutua Muthusi ameeleza kuwa Umoja huo umekua ukitekeleza miradi mbalimbali katika nchi za Afrika na hivyo imeongeza ofisi karibu na Nchi Wanachama ili kuwezesha Sekta ya Posta kuchangia maendeleo ya nchi zao.
“Napenda kuipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuruhusu kuwa na Makao Makuu ya PAPU na Ofisi ya UPU jijini Arusha. Pia napenda kusema kuwa Afrika ni muhimu kwa UPU na hii ni hatua muhimu na ya pekee kwa kuwa sio Jumuiya zote za Kimataifa zinamiliki majengo kama ilivyo PAPU”.