Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Pamoja na Kuelimisha na Kuponya, Tuzuie Changamoto Zisitokee – Waziri Chana
Sep 08, 2023
Pamoja na Kuelimisha na Kuponya, Tuzuie Changamoto Zisitokee – Waziri Chana
Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana akizungumza na Watumishi wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) na kupokea taarifa ya Tume kwa mara ya kwanza baada ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Wizara ya Katiba na Sheria.
Na Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO

Rai yatolewa kwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) kuwa pamoja na utoaji elimu ya kulinda haki za binadamu, kuponya pamoja na kuandika ripoti, waone namna ya kuzuia changamoto hizo zisijirudie au zisitokee tena.

Rai hiyo imetolewa jana jijini Dodoma na Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana wakati akizungumza na Watumishi wa Tume hiyo na kupokea taarifa ya Tume kwa mara ya kwanza baada ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Wizara hiyo.

Pamoja na rai hiyo, Waziri Chana ameitaka Tume kutenga bajeti kwa ajili ya kuendelea kujenga majengo ya Ofisi za Kanda na kuweka mikakati ya kumaliza changamoto ya upungufu wa watumishi wa tume hiyo.

“Kuhusu mkakati wa kuendelea kufungua Ofisi za Kanda, tunatakiwa tufahamu kwamba Tume ni chombo cha kikatiba, hivyo ofisi hizo haziwezi kuendelea kuwa za kukodisha, ni lazima kuwa na Makao Makuu na Ofisi za Kanda za uhakika, vile vile, tuweke mikakati ya watumishi kwani ni lazima kuona ni namna gani ya kuongeza nguvu hususan upande wa Ofisi za Zanzibar maana nguvu kazi ndio kipaumbele”, alisema Waziri Chana.

Akiongelea kuhusu bajeti, Waziri Chana amesema, wameshaanza kuweka mikakati ya namna ya kuendelea kuwa na bajeti ya kutosha pamoja na mikakati ya kupata wadau watakaosaidia baadhi ya shughuli za wizara bila kuingilia masuala ya nchi wala kutoa masharti magumu.

Aidha, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa nafasi hiyo na kuahidi kuwa katika kipindi ambacho amepewa dhamana ya kuiongoza wizara hiyo atahakikisha anaitendea haki dhamana hiyo kwa kutenda haki, kujadiliana, kupanga, kusomanisha mifumo na kufanya kazi kwa pamoja na watumishi.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Mstaafu Mhe. Mathew Mwaimu amesema kuwa, tume ilianza na salio la malalamiko 1524 na ilipokea malalamiko mapya 150 hivyo kufanya jumla ya malalamiko yaliyokuwa yanashughulikiwa na Tume kuwa 1,674 ambapo hadi kufikia mwezi Juni 2023, Tume ilikuwa imeshughulikia malalamiko 789 na kuyahitimisha.

“Kwa kipindi husika, kwa kuzingatia upatikanaji wa rasilimali fedha na lalamiko husika, Tume imefanya chunguzi maalum kumi kwa kwenda uwandani kukusanya ushahidi na vielelezo ili kupata ukweli wa tuhuma ambapo taarifa hizo za chunguzi zimekamilika na zimewasilishwa kwenye mamlaka husika kwa mujibu wa sheria kwa ajili ya utekelezaji wa mapendekezo ya Tume”, alisema Jaji Mwaimu.

Jaji Mwaimu ameongeza kuwa katika kipindi hicho, Tume imeendelea kutoa elimu kwa umma kwa kutumia njia mbalimbali zikiwemo za kushiriki katika maadhimisho mbalimbali, kugawa machapisho, makongamano, vipindi vya redio na luninga, mikutano, matangazo, matamko na kupitia klabu za haki za binadamu 301 katika shule za sekondari, vyuo vya kati na taasisi za elimu ya juu.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi