Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Ofisi ya Ardhi Mara Kuwezeshwa Vifaa vya Upimaji
Mar 31, 2020
Na Msemaji Mkuu

[caption id="attachment_51916" align="aligncenter" width="750"] Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula akikagua ofisi mpya za ardhi mkoa wa Mara wakati wa ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi mkoani Mara jana. Kulia kwa Naibu Waziri ni Mkuu wa Wilaya ya Musoma Dkt. Vincent Naano Anney na Kulia ni Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Mara Jerome Kiwia.[/caption]

Na Munir Shemweta, WANMM Musoma

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt Angeline Mabula amesema wizara yake itaipatia Ofisi ya Ardhi Mkoa wa Mara vifaa vya upimaji ili viweze kutumiwa na halmashauri za mkoa huo  kwa lengo la kuongeza kasi ya upimaji.

Dkt. Mabula alitoa kauli hiyo jana wilayani Musoma Mkoa wa Mara alipokwenda kukagua ofisi mpya ya ardhi ya mkoa Mara ikiwa ni jitihada za wizara ya ardhi kusogeza huduma za ardhi kwa wananchi.

Awali huduma za ardhi zilikuwa zikitolewa na ofisi za Mkamishna Wasaidizi wa Kanda ambapo kanda moja ilikuwa ikihudumia zaidi ya mikoa miwili jambo lililokuwa likiwapa usumbufu wamiliki wa ardhi kwenda umbali mrefu kuifuata huduma hiyo.

Alisema, baada ya wizara yake kuanzisha ofisi za mikoa sasa wananchi watapata huduma za ardhi katika mikoa husika na migogoro ya ardhi sasa itapatiwa ufumbuzi kupitia wataalam watakaokuwa katika mikoa hiyo.

[caption id="attachment_51918" align="aligncenter" width="750"] Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Mara, Jerome Kiwia akimuonesha Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula sehemu ya Ofisi mpya za ardhi Mkoa wa Mara wakati Naibu Waziri alipokwenda kuzikagua ofisi hizo mkoani Mara jana. Kulia kwa Naibu Waziri ni Mkuu wa Wilaya ya Musoma Dkt. Vincent Naano Anney.[/caption]

Alibainisha kuwa, katika jitihada za kuongeza kasi ya upimaji maeneo mbalimbali ofisi za mikoa zitapatiwa vifaa vya upimaji ili visaidie halmashauri kupanga, kupima na kumilikisha ardhi na kusisitiza vifaa hivyo vitatolewa bure na aliwataka wakurugenzi wa halmashauri kushirikiana na ofisi za ardhi za mikoa.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri Mabula, Wizara yake imeamua kubeba jukumu la kutoa vifaa vya upimaji ili kuongeza kasi ya upimaji ingawa jukumu hilo linapaswa kufanywa na halmashauri kwa kuwa ndizo zenye mamlaka za upangaji miji katika maeneo.

Dkt. Mabula amesikitishwa na kiasi kidogo kinachotengwa na Halmashauri kwa ajili ya kazi za kupanga, kupima na kumilikisha ardhi ambapo alitolea mfano wa Halmasahauri ya Musoma kutenga milioni 30 kwa kazi mbalimbali za sekta ya kiasi alichokieleza kuwa  kidogo.

“Milioni 10 au 15 utapima viwanja vingapi? Halmashauri hazijaipa kipaumbele sekta ya ardhi ndiyo maana malalamiko yanakuwa mengi, muongeze bajeti za upimaji’’ alisema Dkt. Mabula

Hata hivyo, ameishauri Halmashauri ya wilaya hiyo kuwatumia wataalam wake kwa kuandika andiko ili kupatiwa mkopo usio na riba unaotolewa na wizara kwa ajili ya shughuli za umilikishaji ardhi ambapo alisema katika kipindi cha bajeti ijayo wizara inatarajia kupata shilingi bilioni saba kwa ajili ya kuzikopesha Halmashauri.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya hiyo Dkt. Vincent Naano Anney aliipongeza Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa uamuzi wake wa kuanzisha ofisi za mikoa na kueleza kuwa uamuzi huo utaleta nafuu kwa wananchi katika kupata huduma za ardhi ambapo awali iliwalazimu kusafiri hadi Simuyu kupata huduma hiyo.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi