[caption id="attachment_6055" align="aligncenter" width="750"] Mbunge wa Sengerema Mhe. William Ngeleja (kushoto) akionesha nakala ya malipo ya kiasi cha shilingi milioni 40.4 alizozirejesha Serikalini kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) fedha alizopewa kama msaada toka kwa Bw. James Rugemalira wa Kampuni ya VIP Engeneering and Marketing Ltd. Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari Bi. Zamaradi Kawawa[/caption] [caption id="attachment_6058" align="aligncenter" width="750"] Mbunge wa Sengerema Mhe. William Ngeleja (kushoto) akifafanua jambo kwa Waandishi wa Habari (hawapo pichani) wakati akitoa taarifa ya kurejesha kiasi cha shilingi milioni 40.4 Serikalini kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), fedha alizopewa kama msaada toka kwa Bw. James Rugemalira wa Kampuni ya VIP Engeneering and Marketing Ltd. Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari Bi. Zamaradi Kawawa. Picha zote na Eliphace Marwa[/caption]
Na. Agness Moshi
Baada ya watuhumiwa wa sakata la Akaunti ya Tegeta ESCROW, Bw. James Rugemalila na Bw. Harbinder Singh Seth kukamatwa na kufikishwa mahakamani, hatimaye sakata hilo limechukua sura mpya kufuatia moja ya watu waliofaidika na fedha za akaunti hiyo Bw. William Ngeleja kurudisha fedha Serikalini kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Mhe. Ngeleja ambaye ni Mbunge wa Sengerema na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini ametangaza kurudisha fedha hizo wakati akizungumza na Waandishi wa Habari katika Ukumbi wa Idara ya Habari (MAELEZO) leo jijini, Dar es Salaam.
Ngeleja amesema kuwa mwaka 2014 alipokea kiasi cha shilingi millioni 40.4 kama msaada kutoka kwa mmiliki wa VIP Engineering and Marketing Bw. Rugemalila kupitia account yake namba 00110102352601 ya Benki ya Mkombozi.
“Nilipokea fedha hizo kutoka kwa ndugu Rugemalila bila kujua kwamba fedha hizo zilikua zinahusishwa na kashfa ya akaunti ya fedha ya Escrow kama ilivyo sasa”, alisema Ngeleja
Ngeleja aliongeza kwa kusema kuwa fedha hizo alizipokea kwa nia njema kama msaada au mchango ili zimsaidie katika kutekeleza majukumu yake ya kibunge jimboni kwake, hususani kusaidiana na wananchi katika shughuli za kijamii kama vile shughuli za ujenzi wa shule, makanisa na misikiti pamoja na miradi ya maendeleo ambayo haipo kwenye bajeti ya serikali.
Mbunge huyo amezitaja sababu za kufikia uwamuzi wa kuzirudisha fedha hizo Serikalini ni pamoja na kujiridhisha kuwa aliyempa fedha hizo ni mtuhumiwa kwenye kashfa ya ESCROW.
“Nimepima na kutafakari na hatimaye nimeamua kwa hiari yangu mwenyewe kurejesha serikalini fedha zote nilizopewa kama msaada bila kujali kwamba nilishazilipia kodi ya mapato”, alisema Ngeleja.
Aliongeza kuwa amerudisha fedha hizo ili kulinda heshima yake na maslahi mapana ya nchi, chama chake na wananchi wa jimbo lake. Lakini pia yeye akiwa kama kiongozi wa umma kwa miaka ya miaka 12 hakuwahi kukumbwa au kuhusishwa na kashfa ya ufisadi au rushwa. “Nimesononeka na kufadhaika sana kuona kuwa msaada niliopewa sasa unahusishwa na tuhuma”, aliongeza Ngeleja.
Ikumbukwe kuwa sakata la ESCROW lilianza mwaka 2014 likihusisha ubadhilifu wa jumla za fedha kiasi cha shilling billioni 306 ambapo zilitolewa Benki kuu ya Taifa (BOT) na kugawanywa kwa watumishi wa umma, wafanyabiashara na viongozi wa dini.
Mhe. Ngeleja akiwa kama mmoja wa wanufaika wa fedha hizo alisema kuwa hajutii kupokea msaada kwani kupokea msaada ni jambo la kawaida kwa viongozi lakini msaada ukibainika na harufu ya uchafu hata kama haujathibitishwa na vyombo vya husika ni vyema kujiepusha nao.