Na Mwandishi wetu
Tume ya Taifa ya Uchaguzi imewasihi wapiga kura wote waliojiandikisha kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na wanaoishi kwenye Jimbo la Liwale mkoani Lindi na kata nne za Tanzania Bara, kujitokeza kwa wingi kupiga kura siku ya Jumamosi Oktoba 13 mwaka huu ili kuwachagua viongozi wanaowataka wawaongoze kwa kipindi cha takribani miaka miwili ijayo.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Jaji Semistocles Kaijage wakati akisoma risala ya uchaguzi mdogo wa jimbo hilo unaohusisha pia kata za Kibutuka katika Halmashauri ya Liwale, kata ya Korongoni katika Halmashauri ya Manispaa ya Moshi na Kata za Majengo na King’ori katika Halmashauri ya Meru.
Amewataka kwenda kupiga kura bila hofu, woga, wasiwasi au ushawishi kwani chini ya Kanuni ya 3.1 (b) ya Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015, Serikali imepewa wajibu wa kuhakikisha kuwa kuna hali ya usalama, amani na utulivu katika kipindi chote cha Uchaguzi.
Mbali na wito huo, Jaji Kaijage amewataka wananchi, vyama vya Siasa na wadau wote wa uchaguzi kushirikiana ili kuhakikisha kuwa viashiria vya kuvunjika kwa amani na utulivu vinaepukwa ili uchaguzi utakaofanyika uwe huru, wazi na wa haki.
Jaji Kaijage amevisisitiza vyama vya siasa kuwa mikutano ya kampeni inatakiwa kufikia mwisho leo Ijumma saa kumi na mbili kamili (12:00) jioni na baada ya muda huo, vyama, wagombea na mashabiki waache kufanya kampeni za aina yoyote, kama vile kutumia alama za vyama zinazoashiria kampeni, vipeperushi, bendera, mavazina vitu vingine visivyokubalika katika siku ya Uchaguzi.
“Aidha, wananchi waheshimu Sheria za Nchi wakati wote wa upigaji, kuhesabu, kujumlisha kura na kutangaza matokeo. Pale panapokuwa na malalamiko yoyote ya ukiukwaji wa Sheria na Taratibu za Uchaguzi, malalamiko hayo yafikishwe kwenye mamlaka inayohusika kwa utaratibu uliowekwa kwa mujibu wa Sheria.”, amesema Jaji Kaijage na kuongeza kuwa:
“Vivyo hivyo, Viongozi wa Vyama vya Siasa, Wagombea au wafuasi wao na wananchi kwa ujumla wajiepushe na vitendo vinavyoweza kusababisha fujo au vurugu katika vituo vya Kupigia, Kuhesabia na Kujumlishia Kura.”
Jaji Kaijage amewataka wapiga kura kuondoka kwenye maeneo ya vituo vya kupigia kura mara baada ya kupiga kura na kujiepusha na mikusanyiko au mikutano katika maeneo ya vituo vya kupigia kura kwani vyama vya siasa vimeweka mawakala vituoni ambao watalinda maslahi ya vyama husika na wagombea wao.
Mwenyekiti huyo wa NEC, amevikumbusha vyama vya siasa, wagombea, wananchi na watendaji wa uchaguzi kwa ujumla kuzingatia na kuheshimu matakwa na masharti ya Sheria za Uchaguzi, Sheria za Nchi, Kanuni na Maadili ya Uchaguzi wakati wa Upigaji Kura, Kuhesabu, Kujumlisha Kura, na Kutangaza matokeo.
Amesema upigaji kura utafanyika kuanzia saa moja kamili asubuhi na kumalizika saa kumi kamili jioni katika vituo vilivyotumika wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na kwamba watakaokuwepo kwenye mstari kwenye vituo vya kupigia kura kuanzia saa kumi kamili jioni wataruhusiwa kupiga kura.
Hata hivyo, amebainisha kuwa watakaoruhusiwa kupiga kura ni wale tu waliomo kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwenye Jimbo au Kata husika na wana kadi ya mpiga kura na wale waliopoteza kadi zao za kupigia kura au zimeharibika au zimechakaa wataruhusiwa kupiga kura kutumia Pasi ya Kusafiria, Leseni ya Udereva au Kitambulisho cha Uraia kinachotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) kwa sharti kuwa majina yaliyomo kwenye vitambulisho hivyo yafanane na yale yaliyomo kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
“Ni wajibu wa vyama vya siasa vinavyoshiriki katika uchaguzi kuweka mawakala katika vituo vyote vya Kupigia na Kujumlishia Kura kwa utaratibu ambao tulikubaliana na umekuwa ukitumika katika chaguzi za hivi karibuni wakati wa Mkutano wa Tume na Vyama vya Siasa tarehe 10/07/2018 uliofanyika katika ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere Jijini Dar es Salaam, na maelekezo kuhusiana na utaratibu huo kutumwa kwa Wasimamizi wa Uchaguzi.”, amekumbusha Jaji Kaijage.
Hata hivyo, amesema mawakala hao wanaruhusiwa kuwepo katika Vituo vya Kupigia Kura na wanatakiwa kufuata na kuzingatia Sheria, Kanuni na taratibu zinazoongoza Uchaguzi katika kipindi chote cha kupiga, kuhesabu, kujumlisha kura na kutangaza matokeo.
Uchaguzi huu Mdogo wa Ubunge katika Jimbo la Liwale na Udiwani katika Kata nne za Tanzania Bara, unafanyika kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kujiuzulu kwa mbunge na madiwani wa kata hizo na utahusisha wapiga kura 69,232 walioandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na kutakuwa na Vituo vya Kupigia Kura 192.