Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 30 Julai, 2021 ameongoza Watanzania katika mapokezi ya Ndege mpya aina ya Bombardier Dash 8 Q400 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Kuwasili kwa Ndege hiyo iliyotokea nchini Canada kunaongeza idadi ya Ndege zilizonunuliwa na kuwasili kufikia 9 kati ya 11, Ndege nyingine 2 zinatarajiwa kuwasili mwezi Oktoba 2021.
Akizungumza wakati wa hafla ya kupokea Ndege hiyo, Mhe. Rais Samia amesema usafiri wa anga ni kichocheo muhimu cha maendeleo Duniani kwa sababu usafiri huo ni wa haraka, salama na wenye kutumiwa na watu wengi.
Mhe. Rais Samia amesema mbali na usafiri wa anga kusafirisha Watu, pia ni muhimu katika kusafirisha bidhaa mbalimbali, hususan zinazoharibika haraka kama vile matunda, mbogamboga, samaki, maua, nyama na nyinginezo.
Amesema Serikali imeamua kununua Ndege ya kusafirisha mizigo kwasababu nchi yetu ni miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa matunda, mbogamboga na maua, ambapo mwaka 2019, Tanzania iliuza Nje mazao yenye thamani ya takriban Dola za Kimarekani milioni 700 na ina tarajia hadi kufikia mwaka 2025 kuingiza Dola za Marekani bilioni 2.
Aidha, Mhe. Rais Samia amesema ili nchi iweze kuvutia watalii wengi na kunufaika nao ni lazima iimarishe usafiri wa anga na ndio sababu Serikali iliamua kufufua Shirika la Ndege la ATCL ikiwa na malengo ya kupokea watalii milioni 5 ifikapo mwaka 2025 kutoka watalii milioni 1.5 mwaka 2019.
Amesema Serikali imeamua kuimarisha huduma za usafiri nchini ili iweze kunufaika na fursa za kijiografia za kupakana na nchi 8, ambapo kati ya hizo 6 hazina Bahari.
Mhe. Rais Samia amezihimiza Wizara za Viwanda na Biashara, Wizara ya Uwekezaji na Sekta Binafsi kuweka mikakati ya kunufaika na fursa hizo ikiwemo kuanzisha kongani za kiuchumi kwenye maeneo ambapo miundombinu ya usafiri inajengwa.
Vilevile Mhe. Rais Samia ameipongeza ATCL kwa kuimarika tangu ilipofufuliwa ambapo idadi ya watu wanaosafiri kwa Ndege za shirika hilo imeongezeka kutoka wastani wa abiria 4000 hadi 60,000 kwa mwezi.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Shirika la ATCL Mhandisi Ladislaus Matindi amesema ATCL imeongeza safari za kimataifa kutoka kituo kimoja cha Comoro hadi saba ambavyo ni Burundi, China, India, Uganda, Zambia, Zimbabwe na hivi karibuni inatarajiwa kuanzisha safari katika miji ya Kinshasa, Lubumbashi, Kalemie, Ndola, Nairobi, Dubai, Muscat, na London.
Mapokezi ya ndege hiyo mpya pia yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, Spika wa Bunge Mhe. Job Ndugai, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Hussein Katanga, Balozi wa Canada hapa nchini Mhe. Pamella O’Donell, viongozi wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi pamoja na viongozi mbalimbali wa dini na vyama vya siasa.
Jaffar Haniu
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu.