Meneja wa Takwimu za Mazingira na Mratibu wa shughuli za Malengo Endelevu kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) Bi. Ruth Minja akisisitiza jambo wakati akifungua warsha ya wadau wa takwimu leo Jijini Dodoma.
Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) imewahakikishia wadau kuwa itaendelea kuzalisha takwimu bora zinazoendana na mahitaji ya wakati na zitakazosaidia Serikali katika kupima utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu na mpango wa pili wa maendeleo hapa nchini.
Akizungumza wakati akifungua warsha ya wadau wa takwimu inayofanyika mjini Dodoma, Meneja wa Takwimu za Mazingira na Mratibu wa shughuli za Malengo Endelevu kutoka NBS Bi. Ruth Minja amesema kuwa Dhamira ya Ofisi hiyo ni kuhakikisha kuwa wanazalisha takwimu zenye ubora kwa kuzingatia mahitaji.
''Takwimu zinatumika kupima utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu na mpango wa pili wa maendeleo hivyo ni vyema tukawajengea uwezo wadau kutoka katika Majiji na Halmashauri ili tuweze kufanya tathmini ya utekelezaji wake kwa urahisi". Alisisitiza Bi Minja.
Sehemu ya washiriki wa mafunzo ya wadau wa takwimu wakiwemo kutoka katika halmashauri na majiji hapa nchini, mafunzo hayo yamefanyika jijini Dodoma.
Akifafanua Bi. Minja amesema kuwa lengo namba 11 la maendeleo endelevu ni kuweka miji na makazi ya binadamu kuwa salama na yenye maendeleo endelevu hali iliyochochea kufanyika kwa mafunzo hayo kwa wadau.Kwa upande wake mshauri mwelekezi kutoka shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP) Bw. Ambrose Mugisha amesema kuwa anapongeza utendaji wa pamoja katika kufanya tathmini na utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu.
Aliongeza kuwa nchi zinaowajibu wa kushirikiana katika kupiga vita umasikini kupitia utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu.
Naye mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa mazingira (NEMC) Bw. Julius Edward amesema kuwa wadau wote wa mazingira wanalo jukumu la kusimamia utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu.
Ofisi ya Taifa ya Takwimu imekuwa ikiendesha mafunzo yakuwajengea uwezo wadau katika mbalimbali wa takwimu ili waweze kushiriki kikamilifu katika kutumia takwimu kwa maendeleo endelevu na ustawi wa wananchi.
(Picha zote na Daudi Manongi- MAELEZO)