Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Naibu Waziri Ummy Ataka Masuala ya Watu Wenye Ulemavu Kujumuishwa na Kujadiliwa Kwenye Mabaraza ya Mashaurianao
Jan 28, 2021
Na Msemaji Mkuu

Na: Mwandishi Wetu

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Watu wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga amewataka Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kujumuisha na kuweka ajenda za masuala ya wenye ulemavu kwenye Mabaraza ya mashauriano ya Mkoa (Regional Consultative Councils) na Mabaraza ya Mashauriano ya Wilaya (District Consultative Councils) ili kuweza kuhakikishia watu wenye ulemavu wanapata huduma bora, haki na ustawi katika jamii zinazowazunguka.

Hayo yameelezwa wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo mkoani Tabora alipokutana na kufanya mazungumzo na baadhi ya viongozi wa Mkoa huo pamoja na Viongozi wa Shirikisho la Watu Wenye Ulemavu (SHIVYAWATA) katika Mkoa huo.

Mhe. Ummy alibainisha kuwa masuala ya Watu wenye ulemavu yakijumuishwa kwenye mabaraza ya mashauriano ya Mkoa aua Wilaya itasaidia kuibua mikakati ya ujumuishaji, usimamizi na utekelezaji wa masuala ya wenye Ulemavu nchini.

“Katika kuhakikisha kuwa mipango mbalimbali ya Watu wenye Ulemavu inapatiwa ufumbuzi ni bora wakati wa vikao vya mabaraza ya Mashaurianao ya Mkoa na Wilaya mkajumuisha masuala ya kundi hilo maalum, kwa kufanya hivyo itawawezesha kutambua mahitaji yao ya msingi na hamtawaacha nyuma watu wenye ulemavu katika masuala mbalimbali ya kimaendeleo,” alieleza Ummy.

Aliongeza kuwa, bajeti zinapoandaliwa pia kuanzia ngazi ya Mkoa zijumuishe masuala ya watu wenye ulemavu ili kuhakikisha mipango ya kundi hilo ya kimaendeleo inatiliwa mkazo kwa lengo la kuinua kiwango cha utoaji huduma kwa kundi hilo.

Sambamba na hayo, Naibu Waziri Ummy alihimiza juu ya kuimarishwa kwa huduma za afya na zenye staha kwa watu wenye ulemavu ikiwemo upatikanaji wa mafuta kwa wale wenye ulemavu wa ngozi (Ualbino), kuimarisha ulinzi, kuwawezesha watu wenye ulemavu kiuchumi, kuwapatia elimu kwa kuimarisha elimu jumuishi, kujengwa kwa miundombinu fikivu na kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusiana na masuala mbalimbali ya wenye ulemavu.

Aidha, Mhe.a Ummy alitumia fursa hiyo kukemea vitendo vya usafirishwaji na utumikishwaji wa watu wenye ulemavu kuombaomba mitaani na badala yake amewasihi watu wenye ulemavu kuchangamkia fursa ya mikopo inayotolewa na Halmashauri ya asilimia 2% ili waanzishe miradi mbalimbali ya kiuchumi.

kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Dkt. Philemon Sengati kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama, Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha watu wasio waadilifu katika jamii na wenye nia ovu katika kuwatumia watu wenye ulemavu wanachukuliwa hatua.

“Mkoa wa Tabora utaendelea kutoa huduma bora kwa Watu wenye Ulemavu kama sehemu ya utekelezaji wa mikataba na miongozo iliyopo katika kushughulikia masuala ya kundi hilo,” alisema Sengati

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Huduma kwa Watu wenye Ulemavu Ndg. Jacob Mwinula alieleza kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu itaendelea kushughulikia na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili watu wenye ulemavu nchini sambamba na kuhakikisha kundi hilo linapata huduma bora.

Katika Ziara hiyo Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Watu wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga ametembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, Halmashauri ya Wilaya ya Nzega, Halmashauri ya Mji wa Nzega, Halmashauri ya Wilaya ya Igunga lengo ikiwa kupokea taarifa ya ushughulikiwaji, ufuatiliaji na uhamasishaji wa masuala ya kisera, kisheria na miongozo kuhusu huduma kwa watu wenye ulemavu ikiwemo kuwafikia wenye ulemavu vijijini.

Pia, Naibu Waziri alitembelea Chuo cha Ufundi Stadi na Huduma za Marekebisho kwa Watu wenye ulemavu Ruanzali kilichopo Mkoani Tabora.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi