Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Geophrey Pinda amewaasa Watanzania kuhakikisha wanakuwa na mipango bora ya matumizi ya ardhi kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo kwa kuwa ardhi iliyopo haiongezeki na idadi ya watu inazidi kuongezeka.
Mhe. Pinda amesema hayo tarehe 26 Desemba, 2023 nyumbani kwake Kibaoni, Halmashauri ya Mpimbwe mkoani Katavi katika hafla maalum ya chakula aliyowaandalia wananchi na viongozi wa jimbo lake kusheherekea Siku Kuu ya Krismasi.
Katika hafla hiyo iliyohudhuriwa pia na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa na Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda, Naibu Waziri huyo wa ardhi alisema, wakati Serikali ikiandaa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, Watanzania wanatakiwa kuwa na mpango wa matumizi ya ardhi huku wakielewa changamoto kubwa iliyo mbele yao ni kuwa ardhi haiongezeki.
“Miaka 25 inayokuja lazima tufikirie hizi hekta na ekari tulizopewa na Mungu ikaitwa Tanzania inatutoshaje itakapofika miaka 50 ijayo, kwa hiyo ni sisi ndiyo tutakaopanga tutumiaje maeneo yetu”, alisema Mhe. Pinda.
“Kila mtu akikaa ajue ardhi ni yake na ndugu zake kwa hiyo tuishi kwa amani na tusigombane, hakuna namna tutakachokifanya katika eneo hili ni lazima tukubaliane namna ya kuitumia ardhi ndogo katika ongezeko kubwa la watu”. Alisema Pinda.
Akigeukia shughuli za maendeleo kwenye jimbo lake la Kavuu, Mhe. Pinda amewaambia wananchi wake kuwa, jimbo hilo kwa sasa limepiga hatua kubwa ukilinganisha na miaka ya nyuma kwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan amewezesha utekelezaji miradi mbalimbali ya maendeleo hata ile ambayo haikutajwa kwenye Ilani ya CCM na kutolea mfano ujenzi wa zahanati, shule na miundombinu.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mpimbwe, Shamimu Mwariko aliwapa ushauri wananchi wa Mpimbwe kuwa, kama wanataka halmashauri yao ifanane kimaendeleo na halmashauri zilizopiga hatua kubwa kimaendeleo basi wahakikishe wanawashika viongozi wanaofanya maamuzi ya kimkakati.
“Kama kweli mna lengo la kusema sasa sisi Mpimbwe iwe inafanana na eneo fulani shikeni viongozi wanaofanya maamuzi kimkakati, utekelezaji wao, mipango yao ni kuhakikisha wanafungua njia watu waweze kupita njia hizo ndiyo kazi ya kiongozi yoyote duniani”, alisema Shamim.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda yuko jimboni kwake katika Halmashauri ya Mbimbwe mkoa wa Katavi kujumuika wananchi wa jimbo la Kavuu pamoja na mambo mengine kusheherekea Siku Kuu ya Chrismas na wananchi wa jimbo lake.