Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Naibu Waziri Nyongo Asema Serikali Ipo Macho Masaa 24 Kulinda Rasilimali za Madini
Jul 08, 2019
Na Msemaji Mkuu

Na Mwandishi Wetu,

Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo amesema Serikali ipo macho masaa 24 katika siku 7 za wiki na itaendelea kuwabaini kuwakamata na kuwatia hatiani watoroshaji wa madini sambamba na kulinda rasilimali hizo, kwa kuwa watoroshaji hao wamekuwa wakiwahujumu Watanzania  na kurudisha nyuma maendeleo yao.

Akizungumza katika Kongamano baina ya Wadau wa Madini lililoandaliwa na Tume ya Madini kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maendeleo ya Baiashara Tanzania (TANTRADE) leo (Jumatatu Julai 8, 2019) katika Maonesho ya 43 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea katika Viwanja vya Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam, Waziri Nyongo alisema kitendo cha utoroshaji wa madini ni kosa kisheria na hivyo Wafanyabiashara wote wanatakiwa kufuata utaratibu uliowekwa na Serikali.

Kwa mujibu wa Waziri Nyongo katika mwaka wa fedha 2018/19 Serikali kupitia Tume ya Madini imevunja rekodi katika  ukusanyaji wa mapato ya madini hatua iliyotokana na jitihada mbalimbali zilizofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano, ambapo kiasi cha Tsh Bilioni 310 ziliweza kukusanywa hatua iliyotokana na kudhibiti mianya ya utoroshaji wa rasilimali za madini.

“Tangu uhuru nchi yetu haikuwahi kukusanya kiasi kikubwa cha fedha ambacho ni mapato yatokanayo na madini ya kiasi cha Tsh Bilioni 310, hivyo Serikali itaendelea kuweka mkazo kuzuia njia za panya ambazo zimekuwa zikitumiwa na watoroshaji wa madini kutorosha madini yetu na hivyo kuikosesha Serikali mapato” alisema Nyongo.

Aidha Waziri Nyongo alisema katika mwaka wa fedha 2019/2020 Serikali kupitia Tume ya Madini imepanga kukusanya kiasi cha Tsh Bilioni 470 na hivyo aliwataka watendaji wa Tume hiyo kuhakikisha kuwa malengo hayo yanafikiwa kwa kufanya kazi kwa kuzingatia kanuni, sheria na taratibu ikiwemo kuendelea kuwafichua na kuwakamata Wafanyabiashara wasiotaka kufuata sheria.

Naibu Waziri Nyongo alisema Serikali kupitia Tume ya Madini kamwe haitomwonea mfanyabiashara yoyote anayafanya biashara zake kwa kufuata sheria ikiwemo kuuza madini yake katika masoko yaliyofunguliwa na Serikali kwani kwa kufanya hivyo kutawezesha Serikali kukusanya kodi yake pamoja na kuweza kuongeza  mapato ya serikali.

Aliongeza kuwa hadi sasa kuna jumla ya masoko ya madini 29 yaliyofunguliwa katika maeneo mbalimbali nchini na kusema Serikali imeweza mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara kuuza madini katika maeneo hayo katika masoko hayo kwa kuwa ni salama kwao na pia yataiwezesha Serikali kutambua kiasi cha madini kinachozalishwa  na kuuzwa nchini.

Akifafanua zaidi Naibu Waziri Nyongo aliitaka Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) kuendelea kujenga mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara na wadau wa sekta ya madini ikiwemo kuwatafutia masoko na kuwatakutanisha mara kwa mara ili kuweza kutambuana pamoja na kuweza kupeana ujuzi na maarifa mbalimbali.

Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TANTRADE Zanzibar, Latifa Hamisi alisema Ofisi yake itaendelea kuimarisha ushiriakiano na wadau wote wa sekta ya biashara nchini ikiwemo wadau wa madini kwa kuwajengea uwezo sambamba na kuwafutia masoko ya uhakika wa bidhaa zao ndani na nje ya nchi.

Aliongeza kuwa TANTRADE itaendelea kutumia majukwaa yake ya kibiashara ikiwemo mikutano ya mara kwa mara baina yake na Wafanyabiashara pamoja na kutoa mafunzo kwa wafanyabiashara hao ili kuhakikisha kuwa wanakuwa na uwezo wa kuzalisha bidhaa bora zinazokithi masoko ya ndani na nje ya nchi.

Naye Rais wa Shirikisho la Wafanyabiashara wa Madini Nchini (FEMATA) John Bina aliiomba TANTRADE kuweka utaratibu wa kuwatembelea wachimbaji wadogo wa madini katika maeneo mbalimbali nchini ili kuweza kuzitambua changamoto zao kwa kuwa kupitia utaratibu huo utawawezesha kutambua mchango wao katika uzalishaji wa madini na nafasi waliyonayo katika kukuza uchumi wa nchi.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi