Na Immaculate Makilika – MAELEZO, Dar
Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) limetakiwa kuhakikisha kuwa wananchi wa vijijini wanapata habari na kuelimishwa kupitia chombo hicho cha umma kwani ni haki yao kujulishwa kwa wakati kuhusu miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali.
Akizungumza leo wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa TBC jijini Dar es salaam, Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Kundo Mathew amesema kuwa pamoja na chombo hicho kuhimiza yale yote yanayotekelezwa na Serikali wasisahau kuikumbusha jamii juu ya suala la kuilinda na kuienzi amani ya nchi.
“Nitoe rai kwa uongozi wa TBC na watendaji wake kufanya kazi bila uwoga kama Serikali inavyofanya kazi. Mkiona mahali kuna tatizo msisite kuweka hadharani. Mimi nawaunga mkono kwa hilo kwani tutatatua changamoto nyingi za wananchi na kwa haraka zaidi. Pia hiyo ndio njia ya kuisaidia Serikali kurekebisha mambo, kwa kuwa hatuwezi kuwa na taifa ambalo wananchi wake wanaonewa na kunyanyaswa tuu halafu wakose mahali pakusemea”. Amesema Naibu Waziri huyo.
Aidha, amesisitiza “Lazima TBC iwe daraja kati ya Serikali na wananchi wake ili tuchukue hatua za haraka kusaidia wananchi. Niwakumbushe pia kuwa mnayo dhima kubwa na muhimu ya kujenga Taifa letu, kulinda amani na kudumisha utamaduni wetu. Ninawaomba muwe imara katika kuyasimamia hayo”.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TBC, Steven Kagaigai amesema kuwa uwepo wa mabaraza kama hayo sehemu za kazi ni jitihada za Serikali za kushirikisha wafanyakazi na menejimenti kwa pamoja ili kuondoa migogoro sehemu za kazi.
Aidha, mkutano huo wa Baraza la Wafanyakazi wa TBC uliohusisha Wafanyakazi, Wajumbe wa Bodi, Menejimenti na Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi unatajwa kuwa ni baraza muhimu kwa maendeleo ya shirika hilo kutokana na kuwa na majadiliano na hoja zenye lengo la kuboresha utendaji wa TBC pamoja na kupitia utekelezaji wa maazimio ya kikao cha awali.