Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Khamis Hamza Khamis ameongoza Ujumbe wa Tanzania kushiriki Mkutano wa 19 wa Baraza ka Mawaziri wa Mazingira wa Afrika unaoendelea jijini Addis Ababa nchini Ethiopia leo tarehe 17 Agosti, 2023.
Mkutano huo unaofanyika kila mwaka na kuhusisha viongozi hao kutoka mataifa mbalimbali barani humo, unalenga kujadili changamoto za mazingira zinazozikabili nchi za Afrika.
Akizungumzia mkutano huo, Naibu Waziri Khamis amesema nchi hizo zinakutana pia kuandaa misimamo yao kwenye masuala mbalimbali ya kimazingira.
Aidha, amebainisha kuwa viongozi wanafanya maandalizi na kuweka misimamo ya pamoja kuelekea Mkutano wa 28 wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP 28) unaotarajiwa kufanyika Falme za Kiarabu pamoja na ule wa Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEA) unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwaka.
Mhe. Khamis ameongeza kuwa, manufaa ya mkutano huo ni kupeana uzoefu na wataalamu wengine kutoka Afrika kwenye masuala mbalimbali ya kimazingira.