[caption id="attachment_39371" align="aligncenter" width="800"] Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara katika kata ya Mgusu, Halmashauri ya Wilaya ya Geita mkoani Geita akiwasisitiza wananchi umuhimu wa kufuata sheria na kuacha tabia ya kuvamia Hifadhi za Misitu.[/caption]
Na Lusungu Helela - Geita
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Constantine Kanyasu amewaonya wananchi wanaofanya shughuli za kibinadamu ndani ya Hifadhi za Misitu nchini kuacha tabia ya kuwashambulia Watumishi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wanapokuwa wanatekeleza majukumu yao.
Onyo hili linakuja ikiwa zaidi ya watumishi watano wa TFS katika mikoa ya Pwani, Tabora ,Kigoma pamoja Kilimanjaro wakiwa wamepoteza maisha yao kwa kushambuliwa na wananchi wakati wakiwa wanatekeleza majukumu yao.
Aidha, Mhe.Kanyasu amepiga marufuku kwa watumishi wa TFS kujichukulia sheria mkononi kwa kuwapiga wananchi wanapobainika kutenda makosa.
"Watumishi wa TFS hamruhusiwi kumpiga Mwananchi mnapomkamata ndani ya Hifadhi au akiwa anasafirisha mazao ya Misitu kinyume na sheria, atakayebainika sheria itachukua mkondo wake.
Ametoa onyo hilo wakati akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata ya Mgusu wilayani Geita mkoani Geita ikiwa ni ziara yake ya kutatua migogoro ya mipaka kwenye msitu wa Hifadhi Geita iliyopo baina ya Vijiji ambapo jumla ya hekta 4,462.95 zimefutwa kwa tangazo la Serikali.
[caption id="attachment_39372" align="aligncenter" width="800"] Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii,Mhe.Constantine Kanyasu akiwa na kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya ya Geita mkoani Geita akipewa maelezo na Meneja wa Misitu wa Wilaya wa Wakala wa Huduma ya Misitu Tanzania (TFS), Fedy Ndandika wakati alipotembelea eneo la Manga lililokuwa limevamiwa na wakulima ambayo ni moja ya eneo la Msitu wa Hifadhi Geita[/caption]Amesema shughuli za uhifadhi ni lazima zifanyike kwa ushirikishwaji kati ya wananchi na watumishi wa TFS.
" Uhasama unaozidi kujengeka kati yenu hauna tifa katika uhifadhi shirikianeni" amesisitiza Mhe.Kanyasu.
Amewataka wananchi kuheshimu na kuzifuata sheria za uhifadhi ya Misitu nchini huku akiwataka watumishi kujiepusha na migongano kati yao na wananchi.
Katika hatua nyingine, Mhe.Kanyasu amewataka wananchi wafuate sheria kwa kulipia vibali kwa TFS pale wanapokuwa na mahitaji ya mazao ya Misitu badala ya kusubilia mpaka wakamatwe na TFS
Mkuu wa Wilaya ya Geita, Mhe.Josephat Maganga amemueleza Naibu Waziri huyo kuwa hali ya Misitu katika wilaya hiyo ni mbaya kufuatia shughuli za kibinadamu zinazoendelea kufanyika Misitu hiyo.
Hata hivyo, Mkuu huyo wa Wilaya hiyoMhe.Maganga alisema kufuatia hali hiyo tayari Kamati ya Ulinzi na Usalama kwa kushirikiana TFS wameshaanza kufanya doria ya kuwaondoa wafugaji na wakulima waliovamia Hifadhi.
Katika hatua nyingine, Diwani ya Kata ya Mgusu, Pastory Lugusa amemuomba Naibu Waziri huyo kumegewa eneo la Hifadhi kwa vile idadi ya wakazi wa kata hiyo imeongezeka hali inayopelea kukosa maeneo kwa ajili ya malisho na Kilimo.
Kwa upande wake Meneja wa Misitu wa wilaya wa TFS, Fedy Ndandika amemuhakikishia Naibu Waziri kuwa watashirikiana na wananchi hata hivyo tayari wameanza kutoa elimu ya umuhimu wa uhifadhi kwa jamii zinazozunguka Hifadhi.