Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Naibu Waziri Gekul Aihimiza TaSUBa Kuongeza Idadi ya Michepuo
Dec 01, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Pauline Gekul ametoa wito kwa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) kuongeza idadi ya michepuo katika Chuo hicho ili kupata wanafunzi wengi.

Mhe. Gekul ametoa wito huo Desemba 01, 2022 katika Mahafali ya 33 ya Chuo hicho ambapo aliwatunuku Astashahada 121 na Stashahada 96 huku akipongeza uongozi wa chuo hicho kwa kutoa mafunzo bora kwa wahitimu hao.

"Taasisi hii ni ya kipekee hapa nchini na Ukanda wa Afrika Mashariki inayotoa Mafunzo ya Sanaa na Utamaduni na kwa sasa taaluma imeboreshwa ambapo wanafunzi wanaongezeka kila mwaka, hii ni hatua kubwa inayohitaji pongezi, lakini natoa rai kwa chuo kuongeza udahili kwa wanafunzi wa kike", amesema Mhe. Gekul.

Naibu Waziri Gekul, amewaasa wahitimu hao kuwa mabalozi wazuri katika jamii na kutumia taaluma waliyopata kujiajiri na kutumia fursa zilizopo duniani katika fani ya Sanaa na Utamaduni.

Awali, Mkuu wa Chuo hicho Dkt. Herbet Makoye amesema kuwa udahili wa wanachuo kwa mwaka wa masomo 2022/23 umeongezeka na kufikia wanafunzi 835.

Dkt. Makoye ameongeza kuwa mwaka huu wa fedha Taasisi hiyo imetengewa Shilingi milioni 250 kwa ajili ya ukarabati na ununuzi wa vifaa.

"Tumetengewa takriban milioni 150 kwa ajili ya kusimika mitambo ya Runinga na Redio lengo likiwa ni kuanzisha Redio na televisheni ya Chuo", amesisitiza Dkt. Makoye.

Mahafali hayo ya 33 yamejumuisha fani mbalimbali ikiwemo uzalishaji wa Sauti na Muziki, Sanaa za jukwaani, uzalishaji filamu kwa ngazi ya Stashahada na Astashahada.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi