Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Naibu Waziri Aanika Mikakati ya Kukabili Mabadiliko ya Tabianchi
Oct 25, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Khamis Hamza Khamis amesema Serikali imechukua hatua mbalimbali ikiwemo kutekeleza miradi ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Amesema hayo wakati akizungumza kwa nyakati tofauti mkoani Songwe wakati wa ziara ya Kamati ya Mawaziri nane wa Wizara za Kisekta inayoshughulikia migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji.

Akizungumza na uongozi wa Mkoa wa Songwe, Mhe. Khamis alisema Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais inatekeleza miradi hiyo ikiwemo uchimbaji visima katika maeneo yenye ukame ili wananchi waweze kupata maji kwa ajili ya matumizi.

Alisema pia Serikali inatekeleza miradi ya kuwezesha upatikanaji wa majiko banifu ambayo yanasaidia kupunguza au kuondosha kabisa vitendo vya ukataji miti kwa ajili ya kuni na mkaa sambamba na kuhamasisha matumizi ya mkaa mbadala.

Katika kuhakikisha kuwa nchi inaondokana na ukame, zoezi la upandaji miti linaendelea kutekelezwa kwa kupanda miti milioni moja na nusu kwa kila halmashauri.

“Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imeanzisha na inasimamia Kampeni Kabambe ya Hifadhi na Usafi wa Mazingira, Kampeni ya Soma na Mti ambayo inahusisha wanafunzi wa shule na vyuo kupanda miti kwa lengo la kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabanchi,” alisema Mhe. Khamis.

Akizungumza na wananchi wa kitongoji cha Ikanka kijiji cha Itumba wilayani ileje alisisitiza wananchi kuendelea kupanda miti katika maeneo waliyoachiwa ili kutunza mazingira.

Naibu Waziri Chilo alisema kuwa miti mingi inaonekana imekatwa hali inayosababisha ukosefu wa mvua katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Tayari kamati ya Mawaziri nane wa wizara za kisekta imeshatembelea mikoa kumi na tisa kati ya 26 na kamati imeshapeleka mrejesho wa maamuzi ya baraza la mawaziri na inaendelea na ziara yake kwenye mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe na Ruvuma.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi