Adeladius Makwega-WUSM
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, ndugu Saidi Othuman Yakubu Februari 24, 2022 amesema kuwa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Mkandarasi Mjenzi na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Mkandarasi Mshauri waongeze kasi kukamilisha ujenzi wa jengo la wizara hiyo.
“Nasema mna wajibu wa kutimiza majukumu yenu ipasavyo ili kukamilisha ujenzi wa jengo hili kwa wakati kwani Rais Samia Suluhu Hassan ametoa pesa za ujenzi kwa Wizara zote kwa wakati mmoja ni vyema kasi ya ujenzi wa jengo letu iongezeke" Alisisitiza
Akizungumza kwa msisitizo Naibu Katibu Mkuu Yakubu, alisema kuwa anafuatilia kwa ukaribu mno ujenzi wa jengo hilo kuliko hata NHC na TBA wanavyodhani.
“Hapa hakuna utani, lazima kufanya kazi hii kwa haraka na ubora, kwani nimekuwa nikifika hapa kila asubuhi nawakuta wafanyakazi wawili au watatu, huku hata wakati wa kazi watumishi ni wachache mno, ongezeni wafanyakazi na nyie wenyewe mtambue kuwa mpo nje ya muda.” Alisisitiza.
Aliongeza kuwa kwa hali ya ujenzi inavyoendelea Mkandarasa Mshauri (TBA) anapaswa kutimiza wajibu wake ipasavyo na pia kwa Mkandarasi Mjenzi.
Naibu Katibu Mkuu Yakubu aliongeza kuwa utendaji kazi wa NHC na TBA ni kipimo tosha kwa kazi za mbeleni za Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo zikiwamo ujenzi wa viwanja.
Kwa upande wao watendaji wa TBA na NHC waliokuwepo katika eneo la ujenzi walisema kuwa watajitahidi kutekeleza majukumu yao kwa wakati na wameyapokea maelezo ya Naibu Katibu Mkuu Yakubu.