Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Naibu Katibu Mkuu Ataka Halmashauri Kuacha Kubagua Miradi
Oct 24, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dkt. Switbert Mkama ameonesha kutoridhishwa na usimamizi wa Mradi wa Kurejesha Ardhi iliyoharibika na Kuongeza Usalama wa Chakula unaotekelezwa katika Halmashauri ya Nzega mkoani Tabora.

Pia ameshangazwa na namna utekelezaji wa mradi huo unavyosuasua pamoja na kuwa tayari fedha zimeshatolewa na Serikali kwa Halmashauri za Wilaya zinazotekeleza miradi hiyo.

Hayo yamejiri wakati wa ziara ya kutembelea na kukagua Mradi huo katika Maeneo Ukame nchini (LDFS) wilayani Nzega mkoani Tabora.

Alishangazwa na namna wilaya inavyotekeleza miradi ya Serikali kwa ubaguzi kwa kutoipatia kipaumbele miradi ya mazingira kama inavyofanya kwa miradi mingine katika wilaya hiyo.

“Matumizi ya fedha katika mradi huu hayaridhishi hata kidogo, kwa mwaka 2022/23 Nzega mmetengewa Shilingi bilioni 2.3 na kati ya hizo Shilingi milioni 467.6 zipo kwenye akaunti bado hazijatumika na mpaka Disemba zinatakiwa ziwe zimetumika, hali hii hairidhishi hata kidogo,” alisema.

Akiwa ziarani katika Wilaya ya Nzega baada ya kukuta mradi wa ujenzi wa ghala kwa ajili ya kukoboa mpunga unasuasua aliutaka uongozi wa Halmashauri kujitathmini kuhusu utendaji wake na kutoa siku saba wa kuandaa mpango kazi wa utekelezaji wa kazi hiyo.

Katika eneo hilo la ujenzi, Mkandarasi huyo anatajwa kutofanya kazi yake inavyotakiwa ambapo mpaka sasa amechimba msingi pekee wakati Mkataba wake wa mwezi mmoja ulianza tarehe 1 Oktoba, 2022 na unategemea kukamilika 30 Oktoba, 2022. 

“Haiwezekani katika miezi miwili ya mkataba mkandarasi ana siku 23 hajafanya kazi yoyote lakini halmashauri iko kimya, Mkurugenzi yuko kimya, mratibu wa mradi wa wilaya yuko kimya hamchukui hatua,” alisema.

Kutokana na hali hiyo alielekeza kusitishwa kwa mkataba dhidi ya Mkandarasi huyo kwani ameshindwa kutekeleza majukumu yake na kuusimamia mkataba wake na halmashauri.

Aliitaka menejimenti ya halmashauri pamoja kujitathmini katika nafasi zao na kumuondoa mara moja mratibu wa mradi wa wilaya kwakuwa ameshindwa kusimamia mradi huo.

Aidha, katika hatua nyingine alimtaka Mkurugenzi wa Halmashauri kumchukulia hatua Afisa Manunuzi kwa kufanya mchakato wa kununua mashine ya kukoboa mpunga kupitia mradi huo ambayo inadaiwa kutokidhi viwango na kutoendana na bei halisi.

Naibu Katibu Mkuu Mkama alisema mashine hiyo inaonekana imetajwa kununuliwa kwa Shilingi milioni 50 tofauti na viwango na kuelekeza Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Ndani wa Serikali ishirikishwe na kupewa kazi ya kuikagua kujua kama nakidhi viwango.

Kwa upande wake Katibu Tawala wa Wilaya ya Nzega Bw. Evance Chambo alisema amepokea maelekezo hayo na kuahidi kuwa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya itasimamia kikamilifu utekelezaji.

Alisema atamuelekeza mratibu wa mradi wa wilaya awe anatoa taarifa za utekelezaji kila wiki ili kuhakikisha unatekelezwa kama ulivyopanga kuepuka changamoto kama hizo.

Hata hivyo Naibu Katibu Mkuu huyo ametembelea miradi mingine ikiwemo uchimbaji wa visima virefu vya maji katika Kijiji cha Bulende na Bulambukana mradi wa ufugaji nyuki katika kijiji cha Lyamalangwa ambapo amepongeza wanakikundi hao kuonesha hamasa katika ufugaji.

Dkt. Mkama na timu ya wataalamu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais amefanya ziara ya kutembelea na kukagua mradi wa LDFS katika Wilaya za Magu (Mwanza), Nzega (Tabora) na Mkalama (Singida) ambapo ametoa maelekezo baada ya kukutana na changamoto mbalimbali.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi