[caption id="attachment_27455" align="aligncenter" width="1000"] Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt.Harrison Mwakyembe (mwenye suti ya bluu) pamoja na Naibu Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (Wa pili kulia) wakikata utepe kuashiria uzinduzi wa kitabu cha Muongozo kwa Watumiaji wa Huduma na Bidhaa za Mawasiliano leo Jijini Dar es Salaam.[/caption]
Na Shamimu Nyaki
Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe pamoja na Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye wamezindua muongozo kwa watumiaji wa Huduma na Bidhaa za Mawasiliano ulioandaliwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Muongozo huo uliozinduliwa leo Jijini Dar es Salaam una lengo la kuelimisha watumiaji wa huduma za mawasilianoambao umezingatia mabadiliko ya teknolojia na maendeleo katika sekta ya mawasiliano lengo ikiwa ni kuwaonesha watumiaji utaratibu bora wa kufuata ili kufaidika na huduma za mawasiliano ambazo wamezilipia na pia kuondoa changamoto zinazoweza kuleta athari kwa watumiaji wa mawasiliano.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe amesema kuwa watoa huduma wanapaswa kuzingatia kanuni za utangazaji katika kuandaa vipindi vya Radio na Luninga kwa kuzingatia weledi na maadili ya taaluma hiyo bila kumuathiri mtumiaji wa huduma hiyo.
[caption id="attachment_27459" align="aligncenter" width="1000"] Mwanamuziki Mrisho Mpoto na kundi lake wakitoa burudani wakati wa Uzinduzi wa Muongozo kwa Watumiaji wa Huduma na Bidhaa za Mawasiliano uliofanyika leo Jijini Dar es Salaam.[/caption]“Usimamizi wa Kanuni za Utangazaji kwa vyombo vya habari kama wadau wakubwa wa utoaji habari ni lazima usimamiwe na umlinde mtumiaji, lakini pia uwe na manufaa kwa maendeleo ya nchi hasa katika kipindi hiki cha mabadiliko makubwa ya teknolojia,” alieleza Dkt. Mwakyembe.
Naye Naibu Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano Mhe. Mhandisi Atashasta Nditiye ameiangiza Mamlaka ya Mawasilano nchini (TCRA) kuhakikisha Muongozo huo unawafikia watanzania wote ili waelewe namna bora ya kutumia mawasiliano na kuepuka kuingia katika matatizo ya kisheria.
Mhandisi Nditiye ameongeza kuwa ni lazima watumiaji wa mawasiliano kuelewa maudhui ya ujumbe wanaopokea kutoka kwa mtoaji taarifa kabla ya kuufanyia kazi ikiwemo kuusambaza na kuwataka watoa huduma kutoza gharama pasipo kumuumiza mteja.
“Naomba niwakumbushe tena watoaji wa huduma hasa vyombo vya habari kuzingatia maelekezo ya kuendelea kutoa matangazo ya bure kwa zile chaneli ambazo hazitakiwi kulipiwa pindi muda wa maongezi aliolipia mtumiaji katika visimbuzi kuisha na TCRA hakikisheni mnalisimamia hilo” alisisitiza Naibu Waziri.
[caption id="attachment_27460" align="aligncenter" width="1000"] Baadhi ya wadau wa Sekta ya Mawasiliano waliohudhuria Uzinduzi wa Muongozo kwa Watumiaji wa Huduma na Bidhaa za Mawasiliano uliofanyika leo Jijini Dar es Salaam.[/caption]Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Mhandisi James Kilaba ameeleza kuwa muongozo huo unatoa maelezo muhimu kwa watumiaji wa huduma za simu, mitandao, utangazaji pamoja na posta ili kumuwezesha mtumiaji wa huduma za mawasiliano kujilinda na matukio yanayoweza kutokea na kumsababishia athari za kiusalama.
Aidha Mhandisi Kilaba ameongeza kuwa Muongozo huo utamsaisia mtumiaji wa huduma za mawasiliano kufahamu utaratibu wa kuwasilisha malalamiko pale ambapo haki yake itakuwa imekiukwa au pale ambapo hakupokea huduma kwa kiwango ambacho mtoa huduma anapaswa kumpatia.
“Muongozo huu unalengo la kutatua changamoto za watuniaji wa huduma za mawasiliano kupitia vipindi vya redio na luninga, kuandaa makala pamoja na kutoa elimu katika shule kupitia mfumo wa TEHAMA,” alisema Mhandisi Kilaba.
Muongozo huo umejikita zaidi katika wadau wakuu wanne wa Sekta ya Mawasiliano hapa nchini ambao ni Serikali, watoa huduma,watumiaji wa huduma pamoja na Mamlaka ya Mawasiliano nchini ambao ndio wasimamizi na wadhibiti wa mawasiliano.