Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mwigulu: Hatushinikizi Wakimbizi Raia wa Burundi Kurejea Nyumbani
Sep 01, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na: Mwandishi wetu-MAELEZO

Waziri wa Mambo ya Ndani na Elimu ya Uzalendo wa Burundi Pascal Barandagiye amesema maadui wa nchi hiyo wamekuwa wakieneza uongo kuhusu hali ya usalama na amani nchini humo kwa faida zao wanazozijua.

Waziri Barandagiye aliwaeleza waandishi wa habari mwishoni wa Mkutano wa 19 wa Kamisheni ya pande tatu kuhusu wakimbizi wa Burundi uliofanyika jana jijini Dar es Salaam jana kuwa wako wanaoipakazia nchi hiyo kuwa usalama unalegalega na wanadiriki hata kutumia picha ya matukio ya vurugu yaliyotokea nchi nyingine wakidai yametokea nchini humo.

“Burundi ina maadui wengi ambao wamekazania kupotosha ukweli kuhusu hali ya usalama nchini mwetu na wamekuwa wakichukua picha za matukio yaliyotokea nchi zenye machafuko za Afrika Magharibi kuonesha wakidai yametokea kwetu” Waziri Barandagiye alieleza.

Aliongeza kuwa watu hao wamedhamiria sio tu kuchafua taswira nzuri ya nchi hiyo lakini pia kuzorotesha jitihada zinazoendelea za kuleta maelewano nchini humo.

Waziri huyo aliwaambia waandishi wa habari kuwa hali ya usalama nchini Burundi ni nzuri na alitoa wito kwa wakimbizi raia wa nchi hiyo kujiandikisha kwa hiari kurejea nyumbani na kuwahakikishia kuwa Serikali na wananchi wenzao wamejiandaa kuwapokea.

“Tunawahakikishia usalama watakaorejea nyumbani kama tunavyowahakikishia wananchi wote walioko Burundi” alisisitiza Waziri Barandagiye na kuongeza kuwa mali za raia hao zimehifadhiwa na watazikuta salama na kwamba serikali itahakikisha zinarejeshwa kwao.

Kwa miaka mingi Burundi imekuwa ikikumbwa na machafuko ya kisiasa ambayo yamekuwa yakisababisha raia wa nchi hiyo kukimbilia nchi za nje kupata hifadhi wengi wao wakiingia Tanzania.

Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni kutoka UNHCR, hadi 28 Agosti, 2017 kuna wakimbizi wa Burundi karibu 421,800 ambapo asilimia 58.3 yaani wakimbizi 246,008 wanaishi katika makambi ya wakimbizi yaliyoko Tanzania. Wakimbizi wengine wanaishi katika nchi za Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Uganda, Kenya, Malawi na Msumbiji.

Mkutano wa pande tatu ulishirikisha Waziri wa Mambo ya Ndani wa Tanzania na Burundi pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulia wakimbizi (UNHCR).

Katika mkutano huo wajumbe walitia saini makubaliano ya kuwarejesha nyumbani wakimbizi waliojiandikisha kwa hiari na kupitisha Mpangokazi wa utekelezaji wa makuabaliano hayo.

Chini ya Mpangokazi huo wa kipindi cha karibu miezi mine (07 Septemba hadi 31 Disemba, 2017) wakimbizi 12,000 ambao tayari wamejiandikisha kwa hiari watarejeshwa nyumbani huku ukitoa nafasi kwa wengine zaidi watakaojiandikisha kujumishwa.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi