Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mwanri: Kamateni Wafanyabiashara Wanaouza Mbolea kwa Bei Isiyo Elekezi.
Dec 22, 2017
Na Msemaji Mkuu

Na Tiganya Vincent, RS - TABORA

SERIKALI ya Mkoa wa Tabora imeziagiza Kamati za Ulinzi na Usalama za Wilaya kushirikiana na Uongozi wa Halmashauri za Wilaya kuwasaka na kuwakamata wafanyabiashara wa pembejeo ambao wanauza mbolea ya mazao zaidi ya bei elekezi iliyotolewa na Serikali.

Agizo hilo limetolewa jana wilayani Urambo na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wakulima juu ya uwepo wa tatizo la wafanyabiashara kuwauzia mbolea kwa shilingi elfu 50 kwa mfuko wa kilo 50.

Alisema haiwezekani wafanyabiashara waendelee kupuuza maagizo ya Serikali ya kutaka kuuza kwa bei iliyopangwa kwa kuongeza bei nje ya utaratibu rasimu na kama hawataki ni vyema waache kuuza.

Mwanri alisema kuwa kuuza zaidi ya bei elekezi ni wizi la ulanguzi , hivyo watakaobaika kuuza nje ya utaratibu rasmi wakamatwe na wafikishwe Mahakamani.

Aliongeza kuwa watu hao wamekuwa wakiibia Serikali mapato yake kwa kuwa wanachoandika katika stakabadhi ya malipo sio mkulima alicholipa kwake.

Mwanri alisema kuwa pamoja na kuendesha zoezi la kuwabaini wanaoendesha vitendo hivyo ni vema wakaanza kuweka mitengo ya kuhakikisha wafanyabiashara hao hawafichi mbolea ili ionekana kuwa pungufu na kuleta usumbufu kwa wakulima.

 “Haiwezekani Serikali imeshatoa bei elekezi ya mbolea ...kisha wanatokea watu wachache wanajiamulia kupanga bei wanayojua wenyewe huku wakimuumiza mkulima ambaye Serikali imeamua kumshika mkono” alisema Mkuu huyo wa Mkoa.

“Kamateni watu wote wanaondesha vitendo hivyo …la sivyo msipofanya nitawafukuza kazi …kwa wale ambao wako nje ya mamlaka yangu nitapendekeza wafukuzwe kazi, haiwekani wakulima wanaibiwa na wanaleta malalamiko kwenu nyie hamchukui hatua” alisisitiza Mkuu huyo wa Mkoa.

Mmoja wa Wakulima wa wilayani Urambo John Kulwa alisema kuwa hivi sasa wanauziwa mbolea kwa kiwango cha shilingi 50,000/- kwa mfuko wa kilo 50 wakati bei ya Serikali ni shilingi elfu 40,900/-.

Alisema kuwa ukikataa kutoa shilingi 50,000/- hupati mbolea na kwenye stakabadhi ya malipo wanakuandikia bei elekezi.

Kulwa alisema kuwa jambo hilo linawaumiza wao kama wakulima na kuomba ikibidi ufanywe msako wa kushitukiza ili kuwamata.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi