Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

"Mwanasheria Mkuu wa Serikali chunguza hili na mkiona kuna ujinai muweze kuchukua hatua"-Spika Ndugai
Jan 31, 2020
Na Msemaji Mkuu

 

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai

Na. Immaculate Makilika – MAELEZO

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Job Ndugai amemuomba Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dkt. Adelardus Kilangi kulitazama suala Mbunge Zitto Kabwe kutumia nembo ya Bunge katika barua inayotaka Benki ya Dunia kusitisha mkopo wa nafuu wa elimu dola milioni 500 wenye lengo la kuboresha elimu nchini.

Akizungumza leo Bungeni jijini Dodoma katika kipindi cha maswali na majibu, Spika wa Bunge, Job Ndugai alisema kuwa hatua ya Mbunge wa Kigoma Mjini Zitto Kabwe, kuandika barua Benki ya Dunia kwa kutumia nembo ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuitaka benki hiyo isitishe mkopo huo kwa muda ni kutumia vibaya nembo ya Bunge, na kuwa huo si msimamo wa Bunge.

“Katika jambo hili kuna dalili za ujinai, kwa hiyo tunakuomba Mwanasheria Mkuu wa Serikali uchunguze na mkiona kuna ujinai muweze kuchukua hatua, sisi kama wabunge hatujafurahishwa na jambo hili” alisema Spika Ndugai

Spika Ndugai alifafanua kuwa ikiwa Mbunge ana tofauti za kisera ni vyema kurekebisha kwa muktadha huo kuliko kusababisha nchi nzima kukosa fursa kwa sababu tu ya kutokubaliana na jambo fulani.

Kwa upande wake, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Adelardus Kilangi alisema kuwa ofisi yake imepokea maelekezo hayo na itayafanyia kazi kwa mujibu wa sheria zilizopo.

Januari 28 mwaka huu, katika hafla ya kuapisha viongozi mbalimbali iliyofanyika Ikuku jijini Dares salaam, Rais Dkt. John Pombe Magufuli, alisema kuwa Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia alikuja nchini Tanzania mwaka 2019 kwa ajili ya mazungumzo na hivyo wanapotoa hizo fedha wanajua msimamo wa nchi na kuwataka viongozi kutojibishana na baadhi ya watu wanaopotosha kuhusu suala hilo.

 

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi