Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Mwaka Mmoja wa Samia, Ummy Ataja Maeneo 10 ya Kujivunia Afya
Mar 04, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na. Georgina Misama- MAELEZO, Dar es Salaam

Serikali imetoa shilingi bilioni 891.5 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo chini ya Wizara ya Afya, ambapo fedha hizo zimetumika katika maeneo makubwa 10 na kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya Afya nchini.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amebainisha hayo leo Machi 4, 2022 Jijini Dar es Salaam katika mkutano maalumu na Waandishi wa Habari uliohusu mafanikio ya mwaka mmoja wa Serikali ya Awamu ya Sita madarakani.

Waziri Ummy aliyataja maeneo 10 ambayo yalipewa kipaumbele katika mgawanyo wa matumizi ya fedha hizo ambazo hazikuhusisha miradi ya maendeleo iliyosimamiwa na Ofisi ya Rais TAMISEMI na kusema anajivunia maeneo hayo kwani ndani ya mwaka mmoja yameleta mabadiliko makubwa katika sekta nzima ya Afya.

Maeneo hayo ni pamoja na ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya kutolea huduma za afya katika Hospitali za Rufaa za Mikoa na Kanda, Hospitali Maalumu na Hospitali ya Taifa Muhimbili  ambapo kiasi cha shilingi bilioni 90.4 zilitolewa kutekeleza mradi huo, ukarabati wa majengo ya kufundishia katika vyuo vya Afya,  ununuzi na usambazaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi kwa ajili ya Zahanati, vituo vya Afya, hospitali za halmashauri na hospitali zilizo chini ya usimamizi wa moja kwa moja wa wizara ya Afya.

Maeneo mengine ni pamoja na ununuzi na usambazaji wa chanjo za watoto, kununua vifaa tiba vya uchunguzi na matibabu ya wagonjwa pamoja na kuimarisha huduma za upatikanaji wa damu.

“Fedha hizo pia zimetusaidia kugharamia posho za wanafunzi watarajali (Interns) 3,518 wa udaktari, udaktari wa meno na wataalamu wengine wa afya ambapo jumla ya shilingi bilioni 49.9 zimetolewa pia kulipia gharama za masomo kwa ajili ya madaktari bingwa (Specialists) na madaktari bingwa Bobezi (Super Specialists) ndani na nje ya nchi”, aliongeza.

Aidha, serikali haikuacha nyuma mapambano dhidi ya UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria ikiwemo ununuzi wa dawa za ARVs sambamba na kuimarisha mapambano dhidi ya ugonjwa wa UVIKO-19 ambapo  huduma za dharura za wagonjwa mahututi na wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum zilipewa kipaumbele.

Kwa upande mwingine waziri Ummy alimpongeza na kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha sekta ya Afya kupata dawa za kutosha na kuahidi kufanya kazi kwa juhudi  ili kuhakikisha watanzania wanapata huduma stahiki.

“Misingi mikuu ya huduma za Afya ni kuhakikisha mgonjwa anapata huduma, nataka huduma zinazotolewa ziendane na uwekezaji  ambao Serikali imeufanya.”

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi