Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Maafa Wapitishwa Bungeni
Sep 13, 2022
Na Jacquiline Mrisho

Na Mwandishi wetu- Dodoma

Muswada wa Sheria ya Usimamizi wa Maafa umepitishwa Bungeni baada ya kujadiliwa na Wabunge.

Akiwasilisha muswada huo Bungeni jijini  Dodoma Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Mhe. George Simbachawene  alisema  katika kipindi cha miaka saba ya utekelezaji wa sheria ya maafa sura ya 242 na kanuni zake za mwaka 2017 kumekuwa na mafanikio mbalimbali yakiwemo kuanzishwa kwa Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa ajili ya kufuatilia mwenendo wa majanga na kuratibu dharura nchini.

Mhe. Simbachawene aliongeza kuwa mafanikio mengine ni kuboresha utabiri wa hali ya hewa, kuanzishwa kwa Baraza la Usimamizi wa Maafa Tanzania na kutoa misaada ya kibinadamu kwa waathirika wa maafa na kufanya ufuatiliaji wa ugawaji wa misaada hiyo kwa waathirika.“

Pia  Ofisi  ya Waziri Mkuu imefanikiwa kusimamia maghala sita ya kikanda ya kuhifadhi misaada ya kibinadamu, kuanzishwa na kujengewa uwezo kwa Kamati za Usimamizi wa Maafa za ngazi ya Mkoa, Wilaya, Kata na Kijiji au Mtaa kupitia mafunzo, kuelimisha, kuhamasisha na kuwawezesha wadau wa maafa kuhusu kuzuia, kujiandaa, kukabili maafa na kurejesha hali baada ya maafa kutokea kwa kutumia njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na matumizi ya vyombo vya habari,”alisema Mhe. Simbachawene.

Pia akizungumzia  Sheria inayopendekezwa kutungwa alieleza kwamba  inalenga kuweka mfumo wa kusimamia maafa kuanzia hatua za kuzuia na kupunguza madhara ya majanga, kujiandaa, kukabili na kurejesha hali endapo maafa yanatokea kwa kuzingatia sera, sheria na miongozo.

“Muswada unajikita katika kuimarisha uwajibikaji wa kila sekta na jamii pamoja na kuimarisha ushirikiano katika kutekeleza afua za usimamizi wa maafa katika ngazi zote ili kuimarisha ustahimilivu kwa maendeleo endelevu,”alieleza.

Katika hatua nyingine, alifafanua kuwa Muswada ulioandaliwa umezingatia kuimarisha utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Menejimenti ya Maafa ya Mwaka 2004 ambayo ndiyo mwongozo wa msingi katika shughuli za usimamizi wa maafa nchini.

“Muswada unapendekeza kufutwa kwa Sheria ya Usimamizi wa Maafa, Sura ya 242 na kupendekeza itungwe Sheria mpya ambayo itaimarisha mfumo wa usimamizi wa maafa nchini kwa kuondoa changamoto za Sheria iliyopo sasa,” alifafanua Mhe. Simbachawene.

Aidha, alibainisha matokeo yatakayopatikana kufuatia kutungwa kwa sheria mpya ya Usimamizi wa Maafa  kama vile kuimarika kwa mfumo wa kitaasisi wa uratibu na usimamizi wa maafa, kuongeza ushiriki wa wadau katika shughuli za usimamizi wa maafa, upatikanaji na ufanisi katika matumizi ya rasilimali na kupungua kwa madhara yatokanayo na maafa kutokana na kuimarika kwa ushiriki wa sekta na uwajibikaji wa wadau katika shughuli za usimamizi wa maafa.

“Kuimarisha uwajibikaji wa kiutendaji wa shughuli za usimamizi wa maafa katika sekta na ngazi zote kutegemea na aina na chanzo cha janga, kiwango cha hatari na ukubwa wa madhara ya maafa, kuimarisha uratibu wa ushirikiano kati ya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar kuhusu usimamizi wa masuala ya maafa na magonjwa ya mlipuko na kuongeza ufanisi wa mfumo wa tahadhari ya mapema na matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano katika usimamizi wa maafa,” alihitimisha.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi