Na: Lilian Lundo – MAELEZO – Dodoma.
Muswada wa Sheria ya Shirika la Simu Tanzania ya mwaka 2017 inatarajia kuleta mabadiliko makubwa ndani ya shirika hilo ikiwa ni pamoja na kuliondoa shirika hilo katika hali ya ufilisi.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano Elias John Kwandikwa wakati wa majadiliano ya muswada huo baina ya wizara hiyo na Kamati ya Bunge ya Miundombinu, leo mjini Dodoma.
“Muswada wa Sheria ya Shirika la Simu Tanzania ya mwaka 2017 itaiondoa TTCL katika usajili wa muundo wa kampuni na kurejeshwa kwenye Mashirika ya Umma ambapo kwa asilimia 100 litakuwa chini ya Serikali,” alisema Kwandikwa.
Ameendelea kwa kusema kuwa baada ya kupita kwa sheria hiyo mabadiliko makubwa yatafanyika ndani ya shirika hilo ambapo Waziri mwenye dhamana ataanza kutoa maagizo na maelekezo kwa shirika hilo ikiwa ni maelekezo ya jumla pamoja na utendaji kazi wa shirika.
Kwa upande wake mwenyekiti wa kamati hiyo Prof. Norman Sigalla amesema, kamati imeshauri sheria iseme uzoefu wa Mwenyekiti wa bodi pamoja na wajumbe wake katika kufanya biashara.
“Kwa kuwa shirika sasa linakuwa la kibiashara hivyo ni vyema mwenyekiti pamoja na wajumbe wa bodi wakawa na uzoefu wa kufanya biashara ili waweze kuliongoza shirika hilo kwa ufasaha,” alifafanua Prof. Sigalla.
Aidha kamati hiyo imeshauri Waziri mwenye dhamana ajikite katika kuangalia utendaji kazi wa shirika pamoja na masuala ya mapato na kuiacha bodi kufanya kazi yake pasipo kuingiliwa.
Vile vile imeshauri kuwa, mwenyekiti wa bodi, wajumbe na wakurugenzi wa shirika hilo waadhibiwe kutokana na utendaji wao wa kazi na si vinginevyo.
Muswada wa Sheria ya Shirika la Simu Tanzania ya mwaka 2017 utafikishwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya kupitiwa na kujadiliwa na Bunge lote. Bunge litakapopitisha muswada huo utapelekwa kwa Rais kwa ajili ya kutiwa saini na kuanza kutumika kama sheria.