Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Bw. Gerson Msigwa, amesema uwepo wa Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari nchini hauna lengo la kuzuia watu kuingia katika tasnia ya Uandishi wa Habari bali inalenga kupatikana kwa huduma bora katika tasnia hiyo.
Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa bodi hiyo leo Machi 3, 2025, Msigwa amesema utafiti uliofanywa na ofisi yake hivi karibuni, ulibaini vyuo vinavyotoa taaluma ya uadishi wa habari nchini Tanzania, vinazalisha zaidi ya waandishi wa habari takribani 500 kila mwaka, hivyo wanahitaji kujengewa uwezo ili kuwa na ubora wakufanya kazi bora.
“Utafiti tulioufanya hivi karibuni tulibaini vyuo vyetu vinazalisha zaidi ya waandishi wa habari 500 kila mwaka, kusoma ni jambo moja lakini watu hao wanahitaji kujengewa uwezo ili kuwa na ubora wa kufanya kazi iliyobora.” Amesema Bw. Msigwa.
Amesema kundi hilo la wanataaluma ni muhimu na linapaswa kupewa kipaumbele katika kuwafanya kuzalisha kazi bora.
“Hiyo inaonesha kuna ongezeko la vijana wengi katika tasnia, na wengi wao wana shahada ya habari na hawapo katika ‘mainstream', hivyo hao watu unadhani watakwenda wapi? Hivyo uwepo wa Bodi ya Ithibati utasaidia kuwafanya wawe bora na kile kinachozalishwa kiwe bora pia, na sio kuwazuia kuwa waandishi wa habari, kama vyuo vinazalisha unadhani wakitoka hapo watakwenda wapi? Lazima tushirikiane kuwasaidia.” Amesema Bw. Msigwa
Amesema ni muhimu kuwajengea uwezo ili waweze kuwa wandishi bora kwani wengi wapo katika vyombo vya habari binafsi vya mtandaoni.
Aidha, ameitaka bodi hiyo kuliangalia kundi ilo la vijana ili waweze kuzalisha kazi zao kwa ufanisi na kuendana na weledi wa uandishi wa habari
Amewataka pia waandishi wa habari kuikitumia chombo hicho ambacho ni muhimu kwao katika masuala yote yanayohusu taaluma ya uandishi wa habari nchini Tanzania.