Bohari ya Dawa (MSD), imewahakikishia wananchi huduma bora zinazokidhi viwango vya Kimataifa kutokana na hatua zilizochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Sita katika kuimarisha utendaji wake.
Akieleza hatua hizo leo Agosti 24, 2023 jijini Dodoma wakati wa mahojiano maalum na Idara ya Habari (MAELEZO), Mkurugenzi Mkuu wa Bohari hiyo, Bw. Mavere Tukai amesema, MSD inatekeleza mradi mkubwa wa ujenzi wa maghala ya kisasa ya kuhifadhi bidhaa za afya katika mikoa mitano ikiwemo Dodoma na Mtwara ambapo mkandarasi ameanza kazi ya ujenzi.
“Mradi huu hapa jijini Dodoma na kule mkoani Mtwara inagharimu shilingi bilioni 39 ikiwa ni sehemu ya mradi wa ujenzi wa maghala matano tuliyopanga kujenga katika Ofisi za Kanda katika mikoa ya Mwanza, Kagera na Dar es Salaam kwa lengo la kuimarisha huduma zetu kwa kuzisogeza zaidi kwa wananchi, kupanua uwezo wa miundombinu yetu hali itakayopunguza umbali wa kufuata bidhaa za afya Dar es Salaam”, amesisitiza Bw. Tukai.
Akieleza zaidi, Bw.Tukai amesema, maghala hayo yatakapokamilika yatakuwa na uwezo wa kutoa huduma kama ilivyo ghala la Dar es Salaam, hivyo uwekezaji huu utakuwa na faida nyingi ikiwemo kupunguza gharama za uendeshaji, kusogeza zaidi huduma kwa wananchi, kupunguza muda wa kufikisha bidhaa za afya kwa watoa huduma, kuwepo kwa mifumo ya kisasa ya TEHAMA na kuongeza uwezo wa kuhifadhi bidhaa za afya kwa kuzingatia viwango vya kimatifa.
Sanjari na faida za uwekezaji huo, Bw. Tukai ameongeza kuwa, MSD imejipanga kujiendesha kibiashara hivyo kutimiza azma ya kunzishwa kwake kwa kutoa huduma bora kwa wananchi na kuzalisha faida itakayosaidia kuimarisha zaidi huduma zake kwa wananchi.
“Hatua hizi zitaenda sambamba na kujiimarisha katika utoaji wa huduma Kimataifa hasa katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) ambazo tuna jukumu la kuzihudumia”, alisisitiza Bw. Tukai.
Aidha, Bw. Tukai amesema kuwa MSD imechukua hatua za kubana matumizi yasiyo ya lazima ili kuongeza tija.
Ujenzi wa Maghala yote matano utakapokamilika unakadiriwa kugharimu Serikali kati ya Shilingi Bilioni 90 hadi 95 za Kitanzania hali itakayoiwezesha MSD kuimarisha zaidi utendaji wake kwa kutumia mifumo ya kisasa zaidi katika utoaji wa huduma zake.