Mikakati iliyowekwa na Bohari ya Dawa (MSD) katika Mwaka wa Fedha 2023/24, inatarajiwa kuimarisha upatikanaji wa bidhaa za afya zikiwemo dawa, vifaa tiba na vitendanishi.
Mikakati hiyo imeelezwa leo na Meneja Mipango, Ufuatiliaji na Tathmini wa MSD, Hassan Ally Ibrahim katika ukumbi wa Idara ya Habari – MAELEZO uliopo jijini Dodoma wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu maboresho ya mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya ikiwa ni mwendelezo wa Taasisi kutoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya taasisi hiyo na mwelekeo wake kwa mwaka wa fedha 2023/24.
“Katika kuimarisha upatikanaji wa bidhaa za afya, kitakachofanyika cha kwanza ni kuhimiza matumizi ya takwimu ili kufahamu mahitaji, wakati na maeneo ambayo bidhaa za afya zinahitajika, maeneo mengine ya msingi ambayo kwa sasa MSD inayafanyia kazi ni kuimarisha mfumo mzima wa ununuzi kwa kuangalia vizuri mikataba ili bidhaa za afya zisikosekane”.
“Vilevle, tutahimiza ushirikiano na wazalishaji wa ndani ambapo tutatoa fursa kwa kuzingatia misingi ya kisheria na kununua bidhaa kutoka kwao,” amesema Meneja Ibrahim.
Ameitaja mikakati hiyo kuwa ni kuimarisha upatikanaji wa bidhaa za afya na miundombinu ya utunzaji wake kupitia fedha zitakazotolewa na Serikali, kuanza uzalishaji wa mipira ya mikono kwa kiwanda kilichopo katika Kijiji cha Idofi, mkoani Njombe ambacho kipo mbioni kukamilika, kuanza kutekeleza miradi ya uanzishaji wa viwanda vya bidhaa za afya eneo la Zegereni, mkoani Pwani na uanzishaji wa viwanda vya Pamba tiba.
Mikakati mingine ni pamoja na maandalizi ya awali ya kutekeleza mradi wa ujenzi wa kiwanda cha kuzalisha dawa pamoja na bidhaa za pamba tiba na kuanza ujenzi wa maghala ya kisasa katika mikoa ya Dodoma, Mtwara na Kagera kwa lengo la kuongeza nafasi za kuhifadhi bidhaa na kuimarisha ubora wa bidhaa za afya, ambapo ujenzi wa maghala hayo unatarajiwa kuanza mwezi Agosti 2023.
Utekelezaji wa majukumu hayo ya MSD unaenda sambamba na utekelezaji wa maelekezo ya maboresho ya utendaji yaliyotolewa na Rais, Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan.
MSD inapitia mifumo yote ya uendeshaji ikiwemo mnyororo wa ugavi, usimamizi na TEHAMA ili kuendana na kasi ya ongezeko la ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za afya vinavyojengwa na Serikali na kuhakikisha malengo ya Serikali katika upatikanaji wa bidhaa za afya yanafikiwa.