Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Blogu ya Idara ya Habari - MAELEZO

Msalato Satellite City Kuwa Mji wa Mfano
Aug 24, 2023
Msalato Satellite City Kuwa Mji wa Mfano
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Dkt Angeline Mabula akizungumza wakati wa uwasilishaji taarifa za wizara yake mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii jijini Dodoma tarehe 24 Agosti, 2023.
Na Munir Shemweta, WANMM

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt Angeline Mabula amesema mradi wa Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi (KKK) katika eneo la Kitelela mkoani Dodoma maarufu kama Msalato Satelite City utakuwa wa mfano kwa matumizi mbalimbali.

Wizara ya Ardhi inatekeleza mradi kwa kutwaa eneo katika mtaa wa Kitelela jijini Dodoma lenye ukubwa wa takriban ekari 971 kwa kulipa fidia, kupanga na kupima eneo kwa ajili ya matumizi mbalimbali ambapo jumla ya viwanja 1,012 vimepimwa.

Akizungumza wakati wa uwasilisha Taarifa ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuhusu Mradi wa Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi kwa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii tarehe 24 Agosti 2023 jijini Dodoma, Dkt Mabula alisema mradi huo utahakikisha huduma mbalimbali zinapatikana katika eneo hilo sambamba na kuzuia ujenzi holela.

Kwa mujibu wa Dkt. Mabula, Wizara ya Ardhi kwa kushirikiana na Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika utekelezaji Mpango Kabambe wa Jiji la Dodoma imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali katika Jiji hilo.

‘’Suala la Kitelela, tunataka mradi huu uwe wa mfano, tunataka mradi usimamiwe na uwe tofauti na miradi mingine’’, alisema Dkt. Mabula.

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii wakifuatilia uwasilishwaji taarifa za Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi mbele ya Kamati hiyo tarehe 24 Agosti, 2023 jijini Dodoma.

Amebainisha kuwa, utekelezaji wa Mpango Kabambe wa Jiji la Dodoma unaendana na malengo yaliyoainishwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya kupanga na kupima viwanja vipatavyo 2,500,000 kwa miaka mitano (2020-2025).

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhandisi Anthony Sanga alisema, kupitia mradi huo wa Kitelela fedha zitakazopatikana zinatarajiwa kutumika kwa ajili ya kuzungushwa kwa kuanzisha miradi mipya kwenye maeneo mbalimbali nchini.

‘’Mradi wa Kitelela tunaufanya kama ‘demo’ na fedha zinazopatikana kupitia mradi huo zitumike kutwaa na kupima maeneo mengine, hii ni moja ya mikakati ambayo wizara inaendelea nayo’’ alisema Mhandisi Sanga.

Awali wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii waliipongeza wizara ya ardhi katika kutekeleza mradi wa kupanga, kupima na kumilikisha ardhi. Hata hivyo, wameitaka wizara hiyo kuhakikisha inadhibiti mapema ujenzi holela na kuacha kusubiri kufanya zoezi la urasimishaji makazi.

‘’Naipongeza Wizara kwa namna ilivyojipanga lakini ni vizuri ikawa ‘pro- active’ hasa kwa ile miji inayokuwa na kuacha kusubiri kurasmisha makazi.‘’ alisema Mjumbe wa Kamati, Shaban Shekilindi ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Lushoto Mkoa wa Tanga.

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Geofrey Pinda kwa upande wake alisema, wizara yake kwa sasa iko kazini na wajumbe wa kamati hiyo wanapaswa kuimani katika masuala mbalimbali inayotekeleza.

‘’Wizara iko kazini, naomba mtuamini ili tuweze kutekeleza majukumu yetu na mwisho wa siku hii migogoro ya ardhi iweze kupungua kama siyo kuisha’’, alisema Pinda.

Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imewasilisha taarifa zake mbili za utekelezaji, mapendekezo ya Kamati Maalum ya Mawaziri Nane wa Kisekta juu ya Utatuzi wa Migogoro ya Matumizi ya Ardhi katika Vijiji 975 pamoja na Utekelezaji wa Program ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi (KKK) mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii.

Mipangilio
Marekebisho ya Mandhari
Marekebisho ya Maandishi