Na Zuena Msuya, Kilimanjaro
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amezindua mradi wa umeme wa Ujazilizi Fungu la Pili kwa Mkoa wa Kilimanjaro na kuagiza kukatwa 10% ya malipo ya wakandarasi Kampuni ya NJARITA na OCTOPUS kwa kutokamilisha Mradi wa Usambazaji wa Umeme Vijijini Awamu ya Pili (REA II) mkoani humo.
Aidha, ameiagiza Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Same kumsaka na kumuweka ndani mkandarasi NJARITA kwa kutokuwepo eneo la mradi.
Dkt. Kalemani alitoa agizo hilo wakati akizindua mradi huo uliofanyika wilayani Same kwa kuwasha umeme katika Kijiji cha Muheza Kata ya Maore, Nasuro Kata ya Mwembe wilayani humo, Julai 29, 2021.
Aidha, aliwawashia umeme wateja waliounganishwa kupitia mradi huo katika Kijiji cha Kifaru wilayani Mwanga, Kijiji cha Nganjoni Wilaya ya Moshi na Kijiji cha Nkweseko Kitongoji cha Kyareni katika Wilaya ya Hai mkoani humo.
Akizungumzia kukatwa 10% ya malipo ya wakandarasi, Dkt. Kalemani alisema kuwa wakandarasi hao NJARITA na OCTOPUS, walipewa jukumu la kutekeleza Mradi wa REA II katika mkoa huo wa Kilimanjaro kwa Makubaliano ya mkataba wa utekelezaji wa mradi huo kwa kipindi cha miezi 24 kuanzia mwaka 2013.
Dkt. Kalemani alisema kuwa wakandarasi hao hawakukamilisha kazi hiyo kwa wakati ulipangwa na walieleza changamoto mbalimbali walizokutana nazo katika kutekeleza mradi huo, na kulazimika kuongezewa muda wa kufanya kazi hiyo, hata hivyo baada ya kuongezewa muda hawakuweza kukamilisha mradi huo kwa wakati.
“Mkuu wa Wilaya na Kamati ya Ulinzi mtafuteni mkandarasi Njalita na awekwe korokoroni kwa sababu hayupo eneo la mradi, pia nawaagiza REA, kukata 10% ya malipo ya kazi yaliyosalia kwa kazi iliyofanywa na wakandarasi NJARITA na OCTOPUS kwa kuwa mpaka sasa hawajakamilisha kazi waliopewa, wakati taratibu zingine za kisheria zikiendelea kufanyika, hatuwezi kuvumilia tena vitu kama hivi wakati malipo yalikuwa yakifanyika kwa wakati!”, alisema Dkt. Kalemani.
Kuhusu Mradi wa Ujazilizi fungu la Pili, Dkt. Kalemani alisema kuwa, utakamilisha usambazaji wa umeme katika vijiji vyote vilivyobaki katika mkoa huo pamoja na kuwawashia umeme wateja waliolipia.
Aliwafafanulia wananchi wa mkoa huo kuwa, mradi huo wa ujazilizi utatekelezwa ndani ya kipindi cha miezi 12 kwa kuwafikiwa wateja wote kwa nyakati tofauti.
Kufuatia mradi huo aliwataka wakazi wa maeneo ambayo bado hayajafikiwa na umeme watayarishe nyumba zao kwa kutandaza nyaya pamoja na kulipia ili kufungiwa umeme kwa gharama ya shilingi 27,000 tu.
Kampuni ya Kitanzania ya Derm imepewa dhamana ya kutekeleza mradi wa ujazilizi katika maeno yote yaliyobaki katika Mkoa wa Kilimanjaro ambapo pamoja na mambo mengine tayari amewasha umeme katika baadhi ya vijiji vya Wilaya ya Same, Mwanga, na Hai huku kazi ikiendelea.
Aidha, mkandarasi huyo ametakiwa kutumia vijana waliopo katika maeneo yanayozunguka mradi kufanya kazi zile zisizo na taaluma maalum ili kila moja ajivunie na kufurahia uwepo mradi huo.
Sambasamba na hilo, wakazi wa mkoa huo wametakiwa kuwa walinzi wa vifaa na miundombinu umeme vitakavyotumika katika kutekeleza mradi huo ili kurahisisha utekelezaji huo na kukamilika kwa haraka na kwa wakati uliopangwa pia ushirikiano kwa mkandarai huo.
Mkoa wa Kilimanjaro kwa sasa una jumla ya Megawati 137 za umeme, matumizi halisi ni Megawati 41 tu, hivyo wakazi wa mkoa huo wametakiwa kuchamkia fursa mradi huo kuweza kutumia umeme wote uliopo katika mkoa huo kwa kufanya shughuli mbalimbali za kujiletea maendeleo na taifa kwa ujumla.