Naibu Katibu Mkuu (Muungano) Ofisi ya Makamu wa Rais, Bw. Abdallah Hassan Mitawi amesema kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa kuta katika Ufukwe wa Mikindani mkoani Mtwara kutasaidia kutatua changamoto ya athari za mabadiliko ya tabianchi zinazowakabili wakazi wa eneo hilo.
Amesema hayo leo Julai 7, 2022 wakati akikabidhi eneo la mradi wa ufukwe wa Mikindani kwa Manispaa ya Mtwara - Mikindani na kwa mkandarasi Kampuni ya Dezo Civil Contractors kwa niaba ya Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Bi. Mary Maganga.
Mitawi amesema mradi huo utahusisha ujenzi wa kuta za kuzuia athari za maji ya chumvi kuingia katika makazi ya wananchi urefu wa zaidi ya mita 790 pia kuta kadhaa zenye urefu wa mita zaidi ya 1,000 zitaingia ndani ya bahari.
“Mradi huu ukikamilika utarejesha haiba ya Ufukwe wa Mji wa Mikindani kwani eneo hili ni la kimkakati na lina historia kubwa ya matukio ya yaliyotokea katika nchi yetu na niwahakikishie wananchi tatizo la maji kuingia kwenye makazi litapungua kabisa,” alisema.
Mitawi alisema mradi huu wenye thamani ya Shilingi bilioni 2.2 unatekelezwa kwa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni mwanamazingira ambaye amekuwa akishiriki mikutano ya kimataifa kuhakikisha changamoto za mabadiliko ya tabianchi zinatatuliwa.
Awali Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara, Bw. Abdallah Malela aliishukuru Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kupeleka mradi huo mkoani humo akisema utasaidia wananchi kukabiliana na changamoto za kimazingira.
Malela aliahidi ushirikiano kwa Mkandarasi na kusema uongozi wa Mkoa utausimamia mradi huo kwa nguvu zote ili uweze kuleta matunda kwa wananchi wa Mtwara Mikindani.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Mhe. Dunstan Kyoba alitoa rai kwa mkandarasi kutoa kipaumbele cha ajira kwa wakazi wa eneo hilo ili wawe sehemu ya mradi na kuwanufaisha.
Kyoba aliahidi kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa katika kuusimamia mradi huo na kuhakikisha unakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa.
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Dezo Civil Contractors, Shekhe Mohamed Bawazir aliahidi kuukamilisha mradi huo kwa wakati uliopangwa na pia kutoa ajira kwa wakazi wa eneo hilo.
Bawaziri alisema kuwa kampuni imepeleka eneo la ujenzi wa mradi wataalamu wachache ambao watafanya kazi ya kitaalamu ambapo kazi zingine zitafanywa na wananchi.
Tafiti mbalimbali zinaonesha kuwa mmomonyoko wa fukwe umekuwa ukiongezeka kwa kasi kwa miaka ya hivi karibuni. Kasi hii imekuwa ikisababishwa na sababu za kiasili kama vile kuongezeka kwa kasi ya upepo unaosababisha kuongezeka kwa ukubwa wa mawimbi ya bahari yenye nguvu.
Aidha, athari za mabadiliko ya tabianchi kama vile kuongezeka kwa ujazo wa maji ya bahari zinachangia pia kuongezeka kwa mmomonyoko wa fukwe za bahari, hivyo mradi huo unaotarajiwa kukamilika baada ya miezi 18 utaleta manufaa.